Badala ya kujenga twabomoa!

16May 2017
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Badala ya kujenga twabomoa!

‘UMAKINIFU’ ni tabia au hulka ya kufanya jambo kwa kufuata taratibu zote, hali ya kuwa makini; utulivu; hali ya kufanya jambo kwa kutulia.

‘Papara’ ni ukosefu wa umakini katika kufanya jambo; hali ya kuwa na haraka na kukosa umakini; pupa, haraka na siku zote “haraka haraka haina Baraka.” Jambo linalofanywa kwa pupa huwa halitengenei au halifani.

Methali hii yatunza umuhimu wa kufanya mambo yetu kwa utaratibu ikiwa twataka mambo hayo yafane au yafanikiwe.

Nasoma ukurasa wa 19 wa gazeti la Jumapili fulani. Makala iliyo chini ya ukurasa huo imepewa kichwa: “Kuunguruma tumbo na mazoezi.” Mwanzo wake umeanza hivi: “wingine kuzusha maradhi mengine ya ganzi na viungo vya mwili kukosa nguvu na kuuma.”

Hapa wasomaji wanaelimishwa nini? Kwanza ‘kuunguruma’ si Kiswahili kwani halimo katika lugha. Neno lililomo ni ‘nguruma,’ hivyo inapokuwa hivyo husemwa ‘kunguruma’ na si ‘kuunguruma!’

Nimeeleza mara nyingi lakini ‘cha kuvunda hakina ubani’ chambilecho (kama walivyosema) wahenga.

Makala ya mwandishi imeanzia katikati na nina uhakika si kosa lake bali ni aliyeandaa ukurasa huo kutokuwa makini na kazi yake. Hapa ndipo maana ya ‘umakini’ unapohitajika kwa wasomaji na waandaaji kurasa.

Ukurasa wa 6 wa gazeti maarufu nchini hivi sasa liliandika hivi: “JPM awaapishwa wajumbe kamati ya madini akiwataka kuzingatia uzalendo.”

Hapa kosa ni la wanaodurusu kwani hawakuwa makini katika kazi yao. Badala ya “JPM awaapishwa …” usahihi ingeandikwa “Wajumbe kamati ya madini waapishwa, watakiwa kuzingatia uzalendo.”

Gazeti hilohilo: “Makocha walivyoina Taifa Stars.” Kwa hakika makocha ‘hawakuina’ Taifa Stars bali ‘waliiona’ Taifa Stars. Ni wapitiaji kutokuwa makini nay ale wanayopitia kuhakiki lugha. Ingekuwa “Makocha walivyoiona Taifa Stars.”

“Kwa mujibu wa daktari wa Yanga, Edward Bavu alisema atakuwa …” Inaposemwa au kuandikwa “kwa mujibu wa …” haiongezewi neno ‘alisema’ kama ilivyoandikwa. Usahihi ni “Kwa mujibu wa daktari wa Yanga, Edward Bavu, atakuwa …” Isemwapo “kwa mujibu wa” maana yake ni kumthibitisha aliyesema.

“Hali hiyo pia ilikuwa kwa Azam FC, wakati mshambuliaji wake wa kimataifa wa Ghana, Mohamed alipolalamika kuumia kwa misuli ya paja.” Jamani! “kuumia ‘kwa’ misuli ya paja” au “kuumia misuli ya paja?”

Kwa nini mwandishi ametumia neno ‘kwa?’ Siku hizi neno hili latumiwa ovyo hata mahali lisipostahiki. ‘Kwa’ ni neno linalounganisha sentensi mbili. ii) neno linalotumika kuhusisha tendo na kifaa kinachotumika kutendea: amelima kwa jembe, anakula kwa kijiko, amesafiri kwa ndege n.k.

iii) neno linaloeleza namna tendo lilivyofanyika: amesoma kwa haraka. Tendo linaloeleza pahali tendo lilipofanyika: amepelekwa kwa daktari. iv neno linalotumika kuunganisha vitu viwili katika kulinganisha: walishindana nyumba kwa nyumba.

Hivyo sentensi ya mwandishi ingeandikwa: “Hali hiyo pia ilikuwa kwa Azam FC, wakati mshambuliaji wake wa kimataifa, wa Ghana, Mohamed alipolalamika kuumia misuli ya paja.” Hakuna sababu ya kuandika ‘paja lake’ kwani hawezi kulalamikia maumivu ya paja lisilo lake.

“Kwa mshangao, Chirwa alipita kwa kasi katikati yao na kuuwahi mpira kisha kuingia katika eneo la hatari kabla ya kuukwamisha wavuni kwa kuugongesha katika nguzo ya juu ya lango na kuzama kimiani dakika ya 70.”

‘Nguzo’ ni kipande cha bomba au mti uliochomekwa ardhini ili kubeba uzito wa paa, dari au nyaya za umeme; mhimili, mwimo. Mpira haukugonga ‘nguzo ya juu’ bali uligonga ‘mwamba’ wa goli.

Sasa tuingie kwenye magazeti ya michezo: “Tambwe karudi matizi bwana.” Kichwa hiki kinaeleza nini? ‘Matizi’ maana yake nini? Tuandike maneno yanayoeleweka mara badala ya kuwafikirisha wasomaji kwani hawana muda huo.

“Matajiri wa Ligi Kuu Bara, Azam msimu huu walifanya uwekezaji mkubwa wa benchi la ufundi na wachezaji lakini sasa wamekiri kuwa watakachopata ndiyo hicho hicho hawana cha kupoteza.”

Samahani mwandishi, husemwa “ndiyo hiyo hiyo” na “ndicho hicho hicho” lakini si “ndiyo hicho hicho” kama ulivyoandika!

Chonde chonde waandishi tusiharibu lugha ya Kiswahili kwa kutumia maneno ya mitaani. “Warembo waliovikwa pete za pesa ndefu.” Kumbe kuna pesa fupi na ndefu eh! Kwani isingeeleweka kuandikwa “Warembo waliovishwa pete za bei ghali?”

Methali: Bila nyuki hupati asali.

[email protected]
0715/0784 33 40 96