Obama, uhamasishaji vimenitoa kiuchumi

24Aug 2019
Gaudensia Mngumi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Obama, uhamasishaji vimenitoa kiuchumi

LINAPOTAJWA jina Barack Obama wapo wanaokumbuka jambo moja pekee nalo ni,  Rais wa zamani wa Marekani. Lakini kwa Tatu Abdallah Mahupa (Tama), sivyo.

Tatu au Mama Tama, akihudumia mteja dukani kwake Tandahimba.

Mwanamama huyu anachokiwaza pale Obama, anapotajwa ni mpenyo mkubwa (mafanikio) alioupata kwenye biashara wakati rais  wa zamani wa Marekani alipoapishwa.

Tatu mfanyabiashara anayeishi Tandahimba mjini mkoani Mtwara hivi karibuni alizungumza na Nipashe iliyokuwa wilayani humo  na kueleza kuwa ujio wa Obama madarakani ulikuwa siku kubwa.

”Nilikuwa mwanamke na mfanyabiashara  wa kwanza Tandahimba kununua runinga, kuiweka uwanjani na kuonyesha watu usiku kucha tukio la kuapishwa Obama huko Washington.”

“Siwezi kuisahau Januari 2009. Ndiyo siku niliyouza bidhaa kuliko siku zote (hakutaja kiasi) niliuza watu walijaa kwenye uwanja wa duka langu kuangalia TV  kuanzia asubuhi saa 4 hadi saa 7 usiku kushuhudia mbashara kiapo cha Obama.Kila kilichorushwa kuhusu Obama nilikitangaza. Hakika niliuza na kupata mafanikio makubwa. “anasema Tatu.

Anasema aliuza soda, vitafunwa, sigara, pipi, chakula na kwa ujumla siku hiyo ilimpandisha chati na kuandika historia katika maendeleo ya wanawake wajasiriamali.

Mfanyabiashara huyu ni maarufu kama Tama, kifupisho cha majina Tatu Abdallah Mahupa, na anachojivunia pamoja na kuwa mfanyabiashara wa kwanza kumiliki na kuonyesha runinga uwanjani huko Tandahamimba, ni kuwa wa kwanza kukodisha viti na maturubai mjini Tandahimba.

Anakiri kuwa ni tofauti na wanawake wengi katika maeneo ya Mtwara na Lindi ambako kuna mfumo dume unaowalazimisha wanawake kutegemea mume kwa asilimia 100, lakini pia ni sehemu talaka holela zilipokubuhu.

Licha ya eneo hilo kuwa maarufu kwa kilimo cha korosho, muhogo na ufuta, kinamama wengi hawana mashamba wala kauli juu ya mazao wanayoshiriki kuyazalisha.

CHIMBUKO MAFANIKIO

Tama anaiambia Nipashe kuwa amehamasika kufanya biashara na kumiliki mali hasa ardhi na ni miongoni mwa wakulima wakubwa waliouza korosho mwaka huu kutokana na mabadiliko na hamasa za kutaka wanawake wagutuke.

‘Nimeuza  kilo 4500 za korosho katika chama cha msingi cha AMCOS Mchichira Leka Tulage.” Anasema Tama na kwamba anamiliki shamba na viwanja pamoja na makazi aliyoyajenga kwa juhudi binafsi.

Anaeleza kuwa alikuwa mjasiriamali tangu akiwa Mbagala jijini Dar es Salaam, huko alikuwa akiuza chapati na kupeleka vitambaa vya nguo za kike nyumbani kwao Tandahimba kuuzia wateja mbalimbali mjini na nje ya mji.

HAMASA KWA WANAWAKE

Tama mwenye miaka 40 anakiri kuwa kampeni zilizofanywa na mashirika mbalimbali ya kijamii kuhamasisha wanawake kuamka kuwekeza ili kubadili maisha yao Tandahimba na maeneo mengine mkoani Mtwara, yanaamsha ari mpya.

Anasema wengi wanamiliki ardhi kutokana na juhudi binafsi na wanajua kusimamia haki zao hasa wale wanaonyanyaswa kiuchumi.

Maelezo yake yanathibitishwa na baadhi ya wanawake wengi wanaosema mkoani Mtwara kuna mwamko wa kujitambua kutokana na mafunzo mbalimbali ya kuwahamasisha kinamama kudai haki zao na kujikita kwenye kwenye ujasiriamali.

Mathalani, hamasa imekuja kutokana na kampeni mbalimbali zilizofanywa na wadau wakiwamo shirika la kimataifa la Action Aid, Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa) ambao wamekemea ukatili na kuhamasisha mabadiliko na hasa kupinga talaka holela na kutelekeza wanawake na watoto.

Akizungumzia uhamasishaji katika ziara ya hivi karibuni iliyofanywa na wanahabari na maofisa wa Action Aid, kuangalia mafanikio baada ya kampeni za uwezeshaji kinamama, Mratibu wa shirika hilo Tandahimba na Newala, Dinno Celestine, anasema:

“Mafunzo yametolewa kukabiliana na unyanyasaji na kudai haki za kinamama, tumewafunza masuala ya unyanyasaji na ukatili  wa kijinsia GBV, pia ukatili dhidi ya wanawake (VAW) na ukatili dhidi ya watoto- VAC na kuwapa mikakati ya kudai na kulinda haki zao na zile za kushirikishwa  kwenye uongozi.”

Wanawake pamoja na kupewa mafunzo ya ujasiriamali na kuanzisha vikundi vya uzalishaji pia wanajizatiti kumiliki ardhi, mazao kama korosho na kufanyabiashara, anaongeza.

Mathalani ziara hiyo ilifika katika kijiji cha Pachoto kilichoko wilayani Newala na kukuta wanawake waliohamasika wakieleza kuwa baada ya mafunzo ya Action Aid, wamewekeza kwenye miradi ya kutengeneza batiki, kulima uyoga, kubangua na kuuza korosho.

Mwaka 2006, shirika hilo la kimataifa katika kupambana na  umaskini  liliwasaidia wanawake wengi kuhamasika na kuanzisha asasi ya kutetea haki zao ya Newora_(Newala Women Rights Association), anasema Mratibu Celestine.

Mwenyekiti wa Newora Wilaya, Sophia Mnalombe, akielezea zaidi anasema asasi hiyo ina wanachama  takribani 8,000 na kwamba kazi za asasi hiyo  zimesambaa katika kata 18 kati ya 24 za wilaya hiyo.

Mnalombe anasema baada ya mafunzo wanajisimamia na kujitetea mathalani wakipewa talaka kiholela wanahoji sababu.

“Zamani wanawake wakitalikiwa walikuwa kimya na waoga hawaulizi sababu za kuachwa kiholela. Siku hizi zama zimebadilika.”

KUTUMIA SHERIA

Aidha, Mnalombe anaeleza kuwa zama hizi  wanasimamia na kuhoji mgawo wa mali za familia kwa misingi ya sharia, mambo waliyojifunza kwenye uwezeshaji na kutumia mgao wanaopata kuanzisha biashara zao.

 “Zamani wanawake walipoachwa wakirudi kwa wazazi wao waliambiwa tumwachie Mungu lakini sasa sivyo. Mwanaume anapotoa talaka mwanamke anataka mgawo wa mali ufanyike kwa maandishi na kuwe na mashahidi,” anasema Mnalombe.

“Tunapotetea haki tunawahamasisha viongozi wa vijiji kushiriki kwenye mazungumzo mathalani watendaji wa vijijji na vitongoji. Wawepo kwenye mashauri mbalimbali iwe unyanyasaji, talaka na kutelekeza familia.Hii imezuia talaka kumwagwa ovyo.”

KAMATI ZA HAKI

Katika kuwawezesha wanawake kudai haki zao Mratibu wa Action Aid, Celestine, anaeleza kuwa kwa kushirikiana na jamii hizo waliunda kamati za vijiji za kutetea haki za wanawake na watoto(VWRC).

Swahiba Gatamo ni mjumbe wa kamati ya Kijiji cha Amani wilayani Newala ya kutetea haki za wanawake na watoto.

Anasema : “Tunaposikia kuna malalamiko tunayafuatilia na kuyafikisha kwa viongozi wa kijiji. Tunachukua maamuzi yao  hadi kwenye ofisi ya mtendaji wa kata. Tunafuatilia kila jambo hatua kwa hatua na kupata ufumbuzi.”

Gatamo anaeleza kuwa wanafuatilia masuala kama kutelekeza watoto, haki za wajane, wanapodhulumiwa na kuwatetea kupitia Newora na serikali za vijiji.

Akizungumzia faida za kuhamasika na kudai haki za kiuchumi na za kibinadamu Fatuma Kassim, ambaye ni mjumbe wa kamati ya haki za wanawake kijijini Pachoto, anasema jukumu mojawapo analofanya ni kusaka taarifa za unyanyasaji kijijini hapo.

“Tukizipata tutandika barua kupeleka taarifa kwa  mtendaji wa kijiji, kata , mahakamani na kwenye ngazi za dini-Bakwata,” anaongeza Gatamo.

Anasema wanafuatilia na kutafuta wanawake wanapotelekezwa, kupewa talaka holela, wazazi kukataa kusomesha watoto, ndoa za utotoni na kufuatilia haki za kielimu kwa wasichana na wanawake kudhulumiwa kwenye familia na ndani ya ndoa

MAFANIKIO KIUCHUMI

Wanawake hawa wanasema kufahamu haki  zao kumeleta mwamko wa kumiliki mali na kufanyabiashara.

“Licha ya kuwa na changamoto kama kunyooshewa vidole kuwa wanawake hawa wanaingilia masuala ya watu, kutishiwa amani na kukosa ushirikiano hasa kutoka kwa wanaofanya unyanyasaji, kwa ujumla kujua haki zetu kumetuwezesha kutoka ndani na kuanza kufanyakazi zinazobadilisha maisha yetu” anasema Gatamo.

Habari Kubwa