Marefa Ligi Z'bar waanzia darasani

24Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
Marefa Ligi Z'bar waanzia darasani

ZAIDI ya waamuzi 65 wa wilaya saba za Unguja wanatarajia kushiriki mtihani wa utimamu wa mwili na masomo darasani na watakaofaulu ndio watakaochezesha mechi za Ligi Kuu visiwani Zanzibar, imeelezwa.

Mtihani huo ambao unatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Amaan visiwani hapa, utatanguliwa na upimaji wa afya zoezi ambalo litafanywa na daktari kutoka Jeshi la Kujenga Uchumi, JKU.

Katibu wa Kamati ya Waamuzi wa Soka Zanzibar (ZAFRA), Muhsini Ali Kamara, alisema mtihani huo utawashirikisha waamuzi wa Unguja pekee kwa kuwa kwa upande wa Pemba wao tayari wameshafanyiwa.

Alisema maandalizi kwa ajili ya mtihani huo yapo vizuri na waamuzi hao baada ya kumaliza mtihani huo wa utimamu wa mwili watashiriki mafunzo ya darasani yatakayofanyika kwa muda wa siku tatu.

 Aidha, alisema mtihani wa utimamu wa mwili utaanza saa 1:00 asubuhi na waamuzi watakaofaulu ndio watakaochezesha Ligi Kuu Zanzibar na si vinginevyo.

Alisema ili mwamuzi aweze kufaulu na kuchezesha ligi, lazima awe amefikia viwango viwili ikiwamo kupasi mtihani wa utimamu wa mwili na masomo ya darasani.