Wanasayansi wabobezi wa mazingira kukutana

24Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Wanasayansi wabobezi wa mazingira kukutana

ZAIDI ya wanasayansi wabobezi wa mazingira 200 wa ndani na nje, watakutana Jumatano ijayo jijini hapa kutathimini na kuweka mikakati ya kuyahifadhi maeneo tengefu nchini.

Wataalamu hao wanakutana katika Kongamano la Kisayansi la Maeneo Tengefu lililoandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), ambalo litafunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), George Simbachawene.

Meneja wa Nemc Kanda ya Kaskazini, Lewis Mtemi, aliwaaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kwamba kongamano hilo limelenga kupitia matokeo mbalimbali ya utafiti na kubadilishana uzoefu wa hatima ya maeneo tengefu nchini.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo ambayo mengi yamekumbwa na athari za kimazingira kuwa ni pamoja na Hifadhi ya Ziwa Manyara, Hifadhi ya Taifa ya Ghuba ya Jozan Chwaka, Bonde la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Mnazi Bay na kisiwa cha Mafia.

 

Mtemi alisema katika maeneo hayo kuna tishio kubwa la kutoweka kwa aina ya viumbe ambao ni adimu katika uso wa dunia.

Alitoa mfano wa kupungua kwa theluji katika Mlima Kilimanjaro, kupungua kwa kina kwa Ziwa Manyara na kumezwa kwa baadhi ya visiwa katika Bahari ya Hindi.

Meneja huyo alisema hatua ya kuingizwa katika maeneo tengefu inatambuliwa na kusimamiwa kwa karibu sana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kutokana na umuhimu wake na kwamba nao watashiriki katika kongamano hilo.

"Lengo ni kujengana kisayansi na kupata maazimio ambayo yatatoa picha halisi na hatimaye kuwasilishwa kwa watunga sera kwa ajili ya utekelezaji kwa manufaa ya taifa," alisema.

Aidha, Mtemi alisema wanasayansi hao pia wataangalia suala zima la mabadiliko ya tabianchi na kuibuka kwa viumbe vamizi katika maeneo tengefu na kuathiri bioanuwai.

Mbali na athari za kimazingira, Mtemi alisema watajadili na kuweka mikakati ya kutumiwa kwa fursa zinazopatikana katika maeneo hayo kwa ajili ya faida za kiuchumi.

Wanasayansi hao wanatoka katika vyuo vya elimu ya juu, taasisi za utafiti na za usimamizi wa uhifadhi, utalii na mazingira zikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa).