Muhongo atumbua kampuni kisa mafuta feki

29May 2016
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Muhongo atumbua kampuni kisa mafuta feki

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameifungia kampuni ya uingizaji mafuta nchini ya Sahara na kuitaka kuondoa mafuta ya ndege (JET A1) iliyoyaingiza nchini yakiwa yamechanganyika na petroli.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo (wa pili kushoto)akitoa maelekezo Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya mafuta ya ORXY alipotembelea visima vya mafuta mbalimbali jijini Dar es Salaam jana. PICHA: MICHAEL MATENANGA

Aidha, ameamuru kuanzia leo, kampuni hiyo isafishe matenki matatu yaliyotumika kuhifadhia mafuta hayo, huku akiagiza kusitishiwa kwa zabuni nyingine zilizotolewa kwa ajili ya kampuni hiyo.

Waziri Muhongo alifikia uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara kwenye kampuni za mafuta ya Puma, Oilcom, Gapco na ORXY kwa ajili ya kuzungumza na viongozi wa kampuni hizo ili kubaini ukweli kuhusiana na mafuta hayo ya ndege.

Muhongo alisema ameamua kuichukulia hatua kampuni hiyo ya Sahara kwa kuwa ni mara ya pili inaleta mafuta ambayo yanakuwa na matatizo.

Waziri aliiagiza kampuni hiyo ianze mara moja kusafisha matenki hayo yaliyohifadhia mafuta ili meli itakapoleta mafuta ipate sehemu ya kuhifadhia na kwamba suala hilo halihitaji mjadala.

“Hatuwezi kusubiria vipimo kampuni zilizopokea mafuta zimesema ni kweli mafuta hayo ya ndege yamechanganyika na petrol… hatuwezi kuendelea kulijadili suala hili na kupoteza muda wakati ukweli unajulikana,” alisema Muhongo

Aliongezea kuwa; “Aliyesababisha haya yote hatujui kama ni yeye ama ni meli. Lakini hii ni biashara yake na anajua tumemsimamisha kwa muda kuingia kwenye zabuni nyingine mpaka hapo itakapobainika ni nani amesababisha jambo hilo. Hatuwezi kupoteza muda… yeye ndiye aliyesababisha. Hata wakisema ni meli imesababisha ,sisi hatujachukua hiyo meli. Jibu linajulikana na hivyo tusipoteze muda,” alisisitiza Muhongo

Alisema kampuni hiyo inatakiwa kuwajibika kwa gharama zao ama kumalizana na wenye meli.

Aidha, Muhongo aliwataka wanaojihusisha na usimamizi wa upakuaji wa mafuta wakubali kupakua aina moja kwa zamu ikiwa watajiona kuwa wanashindwa kupakua aina mbili za mafuta kwa wakati mmoja.

“Kama wangepakua petroli wakamaliza, wakapakua JET A1 wakamaliza, wasingekutana na haya matatizo,” alisema Waziri Muhongo.

Waziri Muhongo alisema pamoja na kutokea kwa tatizo hilo, amewatoa hofu watanzani kwa kueleza kuwa kuna mafuta ya ndege ya kutosha kwa kipindi cha siku 14 kwenye kampuni hizo na kwamba wiki ijayo, kuna meli ya mafuta itaingia nchini.

“Mafuta ya ndege yapo ya kutosha… anayeuza mafuta mengi ni kampuni ya Puma na ameenda kuazima mafuta kutoka kampuni ya Total na kampuni ya ASP ya Rwanda na hayo mafuta yaliyoazimwa yatatumika kwa siku 14, na mengine yataingia Juni 7 mwaka huu. Hivyo hakuna tatizo la mafuta,” alisema Muhongo

Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Michael Mjinja, alisema utaratibu wa kuyaondoa mafuta hayo yaliyochanganyika umeshaanza na walimuita mhusika wa kampuni ya Sahara ambaye aliingia nchini juzi na kumueleza suala hilo.

Alisema hivi sasa wanaangalia eneo ambalo litatumika kuyahifadhi mafuta hayo ili meli ije kuyachukua.

Alisema meli hiyo ilipofika, kulifanyika uhakiki wa ubora wa mafuta hayo na kubainika kuwa yana ubora na hivyo kuruhusiwa kupakuliwa.

Mjinja alisema meli hiyo ilianza kupakua mafuta hayo Mei 4 mwaka huu hadi Mei 8 ilipomaliza na ilipofika Mei 12, ndipo walipopatiwa taarifa kutoka kwenye kampuni hizo kwamba mafuta hayo ya ndege hayana ubora.

“Huenda yakawa yamechangayika wakati yanashushwa kwenye meli kwa sababu kabla ya hapo yalikaguliwa na kuonekana yako safi,” alisema Mjinja

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Felix Ngamlagosi, alisisitiza kuwa pamoja na matatizo hayo, nchi bado ina mafuta ya kutosha kwa siku 14.

Akizungumza wakati akihojiwa na Waziri Muhongo, Mhandisi wa Miradi na Meneja Uendeshaji wa Anga wa Oilcom, Haruna Magota, alisema kampuni yake inakabiliwa na uhaba wa mafuta hayo na kwamba ili kukidhi mahitaji ya wateja wake, inawalazimu kwenda kuazima kwenye kampuni ya mafuta ya Total.

Alisema mafuta ya ndege waliyopatiwa ni lita milioni 8.8 na kwamba mafuta waliyokuwa wameyahifadhi ni lita milioni 2.6, hivyo yote yameharibika baada ya kuchanganyika na hivyo kuwasababishia hasara.

Magota alisema baada ya kuwajulisha wahusika ,waliwataka wasubiri vipimo ingawa tayari imeshabainika kuwa mafuta hayo yana matatizo.
“Hata kama hii kampuni ya Sahara itasema haya mafuta ni masafi, sisi hatutayataka maana vipimo vimeshatueleza ukweli kwamba yamechanganyika na petroli,” alisema Magota.
Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo), aliibua hoja bungeni akisema kuwa akiba ya mafuta ya ndege nchini imebaki ya siku tano, jambo linaloweza kusababisha ndege za kimataifa kushindwa kutua nchini.

“Zimebaki siku tano mafuta ya ndege aina ya JET AI kumalizika nchini baada ya mafuta yote kugundulika kuwa yamechafuka. Sasa baada ya siku hizo, ndege hazitatua nchini na itakuwa ni aibu na nchi itakosa fedha za kigeni kwa watalii kutokuja nchini,” alisema Zitto.

Awali, ilielezwa kuwa kampuni ya Puma ilipatiwa mafuta hayo ya ndege kiasi cha lita milioni 14.4, yenye thamani ya ya Sh bilioni 14.4, kampuni ya Oilcom ilipatiwa lita milioni 10.8 ya Sh. bilioni 10.8 na kampuni ya Gapco lita milioni 2.8 yenye thamani ya Sh .bilioni 2.8.

Habari Kubwa