Yanga nusu makundi Caf

09Apr 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Yanga nusu makundi Caf
  • Kamusoko awanyosha Waarabu wakipoteza muda Taifa, sasa yahitaji sare au ushindi wowote ili…

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga, wamenusa harufu ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya MC Alger ya Algeria katika mechi ya kwanza ya mtoano iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Mshambuliaji wa Yanga, Obrey Chirwa [kushoto],akimtoka beki wa MC Alger, Karaovi Amir katika mechi ya mchujo kuwania kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Yanga ilishinda 1-0. michael matemanga

Thabani Kamusoko ndiye shujaa wa mchezo huo kutokana na kuipatia Yanga bao hilo pekee katika mchezo huo akipiga shuti la kushtukiza akiwa katikati ya 'msitu' wa wachezaji wa MC Alger wakati akimalizia pasi fupi ya Haruna Niyonzima.

Hadi mapumziko hakuna timu ambayo ilifanikiwa kuliona lango la mwenzake, lakini wenyeji Yanga walipoteza nafasi tatu za wazi za kufunga mabao katika mechi hiyo.

Hata hivyo, licha ya MC Alger kuwa nyuma, wachezaji wake walionekana kupoteza muda mara kadhaa bila kujali matokeo ya kufungwa katika mchezo huo uliochezeshwa na Refa Louis Hakizimana kutoka Rwanda.

Dakika ya kwanza Yanga ilifanya shambulizi kupitia kwa Simon Msuva ambaye alipata pasi kutoka kwa Hassan Kessy, lakini beki wa MC Alger Kacem Mehdi aliokoa hatari hiyo langoni mwake.

Dakika ya pili wageni hao walijibu shambulizi hilo kupitia kwa Derarya Warid, lakini kipa wa Yanga, Deogratius Munisi 'Dida' aliwahi kudaka shuti hilo na kuinyima klabu hiyo kutoka Algeria kufunga.

Yanga ilikaribia kupata bao lakini kipa wa MC Alger Chaouch Faruzi alitoa nje shuti lililopigwa na beki wa pembeni wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Haji Mwinyi dakika ya sita huku Dida akidaka shuti la Goveri Kaled katika dakika ya 18.

Dakika ya 25 MC Alger ilipoteza nafasi ya kufunga kupitia kwa Nekkache Hichem ambaye alipiga mpira pembeni akiwa amebaki na Dida peke yake na dakika moja baadaye Obrey Chirwa alichelewa kuunganisha pasi ya Simon Msuva na kuwapa nafasi mabeki wa MC Alger kuokoa.

Katika dakika ya 30, kipa Faruzi alipangua shuti la kushtukiza lililopigwa na Kamusoko na kuinyima Yanga nafasi ya kufunga. Mzambia Chirwa akiwa na kipa alipiga pembeni na kuharibu kazi nzuri ya kuwatoka mabeki wa MC Alger na kupiga shuti hilo akiwa jirani na nyavu.

Kipa Faruzi kwa mara nyingine alipangua shuti la Chirwa dakika ya 85 na kuikosesha Yanga nafasi nyingine ya kupata bao.

MC Alger itaikaribisha Yanga katika mechi ya marudiano itakayofanyika Ijumaa Aprili 14, mwaka huu na mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Yanga: Deogratius Munisi 'Dida', Hassan Kessy, Mwinyi Haji, Nadir Haroub 'Cannavaro', Vicent Bossou, Said Juma, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Obrey Chirwa, Haruna Niyonzima/ Emmanuel Martin ( dk.77) na Deus Kaseke/ Donald Ngoma (dk. 55).

MC Alger: Chaouch Faruzi, Hachoud Abdulrahman, Karaovi Amir, Mebarakou Zidane, Bouhenna Richid, Kacem Mehdi, Chrifei Hichem, Bougueche Hajj/ Feedab Zahir (dk. 81), Derarya Warid, Goveri Kaled/ Seguer Mohammed (dk. 72) na Nekkache Hichem/ Awady Said (dk. 74).

Habari Kubwa