Yanga na sababu Mbao kuiangukia

02Jan 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Yanga na sababu Mbao kuiangukia
  • ***Kuikabili Mlandege leo usiku katika...

BENCHI la Ufundi la Klabu ya Yanga limetoa sababu za kuangukiwa kipigo cha mabao 2-0 na Mbao FC katika Uwanja wa CCM Kirumba juzi, hiyo ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kupoteza dhidi ya timu hiyo tangu imepanda Ligi Kuu Bara.

KOCHA msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa.

Kocha Msaidizi wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, Shadrack Nsajigwa, jana aliliambia Nipashe kuwa kama ilivyo michezo iliyopita dhidi ya timu hiyo ya jijini Mwanza, wamekuwa wakizidiwa ujanja na ndicho kilichotokea juzi.

Alisema Mbao wamewafumbua macho kwa kuwa yapo mapungufu waliyoyaona kwenye kikosi chao na haraka wanaanza kuyafanyia kazi wakiwa Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.

"Kuna makosa ambayo tuliyafanya, kama benchi ya ufundi tumeyaona na mapungufu hayo tunaenda kuyafanyia kazi, hatukutegemea kupoteza mchezo ule, lakini tuwapongeze Mbao walituzidi ujanja," alisema Nsajigwa muda mfupi kabla ya kupanda boti jana mchana kuelekea Zanzibar.

Alisema kikosi chake hakikuwa kwenye ubora wao na kujikuta wakicheza kiwango cha chini na kufanya makosa yaliyotoa nafasi kwa Mbao kuwaadhibu.

Nsajigwa alisema watatumia mazoezi yao kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kuondoa kasoro walizoziona ili kujipanga kwa michezo ijayo ya Ligi Kuu.

Katika mchezo huo wa juzi, Yanga walikosa kasi yao ya ushambuliaji pindi wanapokuwa na mpira na kuwaruhusu wapinzani wao kumiliki mpira zaidi na kucheza soka la kasi wanapounasa mpira na kuwa makini kwenye kukaba wanapopoteza mpira.

Kuwavaa Mlandege leo usikuKatika hatua nyingine, Yanga leo inaanza kutupa karata yake ya kwanza kwenye michuano ya Kombe la Mpinduzi kwa kucheza na Mlandege majira ya saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Amaan.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, aliliambia Nipashe kuwa mara baada ya kuwasili Dar es Salaam majira ya saa 3:25 asubuhi wakitokea Mwanza, waliunganisha na boti ya mchana kuelekea Zanzibar.

"Tupo kwenye boti saa hivi (ilikuwa saa 6:50 mchana) tunaelekea Zanzibar, mchezo wetu wa kwanza ni kesho (leo) usiku," alisema Saleh.

Habari Kubwa