Yanga, Msuva mwaka wao

14May 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Yanga, Msuva mwaka wao
  • ***Wazidi kutisha kileleni, ubingwa, kiatu njia nyeupe...

YANGA imekaribia kuutwaa tena ubingwa baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Mabingwa hao watetezi jana walirejea kileleni baada ya kufikisha pointi 65 sawa na Simba, lakini wakiwa na mechi mbili mkononi wakati mahasimu wao wakibakiza mchezo mmoja.

Simon Msuva aliifungia Yanga bao la kwanza kwa kichwa katika dakika ya saba akiwa katikati ya mabeki wa Mbeya City waliokuwa wameshindwa kumkaba straika huyo ambaye sasa amefikisha mabao 14 akiwa kileleni mwa orodha ya wafungaji Ligi Kuu.

Hata hivyo, baada ya kufunga bao hilo, Msuva hakuweza kunyanyuka kutokana na kuumia kwenye paji la uso maumivu yaliyomfanya atolewe nje kwa machela na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Abdul.

Mbeya City walisawazisha bao hilo katika dakika ya 57 kupitia kwa Haruna Shamte aliyefanikiwa kuwazidi mbinu mabeki wa Yanga ambao walitegea kuufuata mpira wakidhani ameotea.

Mzambia Obrey Chirwa aliunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Abdul na kuipatia Yanga bao la pili katika dakika ya 64.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Yanga kuwa mbele kwa bao 1-0.

Mbeya City ndiyo walikuwa wa kwanza kufanya shambulizi katika lango la Yanga kupitia kwa mshambuliaji wake Zahor Pazi aliyepokea krosi ya Ditram Nchimbi, lakini kipa wa Yanga, Benno Kakolanya alidaka shuti hilo katika sekunde ya 36 na kuwanyima wageni hao bao la mapema.

Kipa wa Mbeya City Owen Chaima naye aliruka na kudaka krosi iliyopigwa na Haji Mwinyi iliyokuwa inaelekea kwenye nyavu na kuwanyima Yanga nafasi ya kufunga katika dakika ya kwanza huku Amissi Tambwe na Chirwa wakishindwa kuunganisha krosi ya Haruna Niyonzima dakika mbili baadaye.

Dakika ya 20 Kakolanya alidaka shuti la Ditram Nchimbi aliyepokea pasi ya Raphael Daudi na kuwakosesha wageni hao nafasi ya kufunga wakati Abdul wa Yanga akiwahi kuokoa hatari langoni mwake na kuitoa krosi iliyokuwa inaelekea kwenye lango lao.

Katika matokeo mengine ya mechi za ligi hiyo iliyopigwa jana, Tanzania Prisons iliichapa Ndanda FC mabao 2-1 katika Uwanja wa Soikoine Mbeya huku Kagera Sugar ikiibuka na ushindi kama huo dhidi ya Mbao FC kwenye mechi iliyopigwa dimba la Kaitaba, Bukoka.

Nayo Mtibwa iliinyuka Mwadui FC 4-2 wakati JKT Ruvu ikilala 1-0 dhidi ya Majimaji.

Yanga: Benno Kakolanya, Hassan Kessy/ Emmanuel Martin (dk. 54), Mwinyi Haji, Nadir Haroub 'Cannavaro' / Kelvin Yondani (dk. 67), Vincent Bossou, Thabani Kamusoko, Simon Msuva/ Juma Abdul (dk. 12), Haruna Niyonzima, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe na Geofrey Mwashiuya.

Mbeya City: Owen Chaima, Haruna Shamte, Hassan Mwasapile, Tumba Lui, Sankani Mkandawile, Ditram Nchimbi, Majaliwa Shabani, Zahor Pazi, Raphael Daudi na Rajab Isihaka/ Mrisho Ngasa (dk. 58).

Habari Kubwa