Yanga kwenye ‘mtihani’ dhidi ya Mbao

29Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Yanga kwenye ‘mtihani’ dhidi ya Mbao
  • ***Yakwea pipa bila ya nyota wake, Chirwa, Ajibu na Yondani…

WAKATI kikosi cha Yanga leo kikitarajia kukwea ‘Pipa’ kuifuata Mbao FC jijini Mwanza, Kikosi hicho cha Kocha George Lwandamina kipo kwenye ‘mtihani’ kutokana na kuwakosa washambuliaji wake nyota, Ibrahim Ajibu na Obbrey Chirwa.

Nyota hao kwa pamoja wameifungia mabao 11 kati ya mabao 17 ambayo Yanga wameyafunga katika michezo yote 11 msimu huu.

Chirwa peke yake amefunga mabao sita huku Ajibu aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Simba amefunga mabao matano na kuisaidi Yanga kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa kwa pointi mbili na vinara Simba.

 

Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Charles Mkwasa, aliiambia Nipashe kuwa nyota hao hawataondoka na timu leo kwa kuwa Ajibu anatumikia kadi tatu za njano huku Chirwa bado akiwa kwao Zambia.

 

Aidha, kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa kukosekana kwa wachezaji hao ni pigo kwao katika mchezo wao huo wa Jumapili lakini lazima wapambane kupata ushindi.

 

“Hatutakuwa nao, ni pigo kwa sababu wamekuwa na mchango mkubwa msimu huu, lakini lazima tujipange na tupambane kupata ushindi,” alisema Nsajigwa.

 

Mbali na kuwakosa nyota hao, Yanga pia itamkosa beki wake ‘kisiki’ Kelvin Yondani ambaye ni majeruhi huku pia ikiendelea kukosa huduma ya kiungo Thaban Kamusoko na Donald Ngoma mabo bado hawajapona majeraha yao.

 

Yanga itakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa Mbao ambao wamekuwa wakiwasumbua wanapokuwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa CCM Kirumba.

Habari Kubwa