Waamuzi Bongo waula Caf

16Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Waamuzi Bongo waula Caf

WAAMUZI wanne wa Tanzania wameteuliwa kuchezesha mchezo wa kuwania nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kati ya Sudan Kusini na Somalia utakaopigwa Aprili 22, mwaka huu

Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika Caf, Ahmad Ahmad

.

Waamuzi hao walioteuliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ni Fredinand Chacha wa Mwanza, Frank Komba na Israel Nkongo kutoka jijini Dar es Salaam.

Refa mwingine aliyeteuliwa katika mchezo huo ni Mfaume kutoka visiwani Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili jana, Chacha alisema ni nafasi nzuri kwao kuiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Alisema wao kama waamuzi wa Tanzania wenye beji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu duniani (Fifa) wako tayari kwa jukumu hilo na wanaamini kufanya kwao vizuri kutawapa nafasi ya kupangiwa michezo mingine.

"Tunashukuru hapa nyumbani tunaonyesha uwezo mzuri na Caf wanatambua taarifa zetu, Watanzania tumepangwa kuchezesha mchezo kati ya Sudan Kusini na Somalia utakaopigwa Aprili 22, mwaka huu huko Djibout.

"Kama waamuzi tunashukuru kuwakilisha nchi katika michuano ya aina hii, lakini ni nafasi kama nchi kuzidi kutambulika kimataifa katika soka na waamuzi wake kupewa nafasi ngumu kama hizi, kwetu ni furaha kubwa sana," alisema Chacha.

Aliongeza kuwa bado wanahitaji kuona waamuzi wengi wanapata beji za Fifa na kupangiwa michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Habari Kubwa