Tenga awataka Stars kufanya kweli Afcon

23May 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Tenga awataka Stars kufanya kweli Afcon

BARAZA la Michezo la Taifa (BMT), limeitaka timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) kwenda kupambana ili kuhakikisha inafika mbali katika Fainali za Kombe la Afrika (Afcon 2019), zitakazofanyika baadaye mwezi ujao nchini Misri.

Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa BMT, Leodegar Tenga, katika semina ya Maofisa wa Michezo inayoendelea jijini hapa.

Tenga alisema wachezaji wa Taifa Stars wanatakiwa kujituma katika kila mechi watakayocheza kwenye hatua hiyo ya makundi kwa lengo la kusaka ushindi utakaowapeleka hatua inayofuata.

Alisema Stars ina kila sababu ya kucheza soka la kiwango cha juu kwa sababu itakutana na timu zenye wachezaji wazoefu katika mashindano hayo.

Tenga alisema wao wakati wanacheza mpira hakukuwa na sapoti kubwa kama ilivyo sasa ambapo wanakila sababu ya kufanya vizuri katika mashindano hayo

Aliongeza kuwa kufanya vizuri katika mashindano hayo, kutawafanya wachezaji hao kujitangaza vema katika ulimwengu wa soka na hatimaye kupata timu kutoka nje ya Tanzania.

"Kikosi kilichoitwa kina wachezaji wazuri ambao wanaweza kujituma wakiwa uwanjani ili kupata matokeo mazuri na kuweza kusonga mbele, inawezekana kufika mbali," alisema nahodha huyo wa zamani wa Stars.

Hata hivyo, aliwapongeza na kuwataka kuwa na moyo wa kujituma na kusikiliza kwa umakini maelekezo ya kocha wao wanapokuwa uwanjani na kutowahofia wapinzani wao kwa kuangalia rekodi walizonazo.

Stars iliyopo Kundi C pamoja na Algeria, Senegal na Kenya inatarajia kuingia kambini Juni Mosi na itaondoka nchini mapema kwenda Misri kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji hao itakayochezwa Juni 13, mwaka huu, katika mji wa Alexandria.