Tambwe aivulia  kofia Mbao FC

02Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Tambwe aivulia  kofia Mbao FC

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Amissi Tambwe, amesema kipigo cha juzi, pamoja na mambo mengine wapinzani wao waliwakamia sana kitendo ambacho kiliwanyima fursa ya kucheza soka lao.

Amissi Tambwe

Tambwe, ambaye huo ulikuwa mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu  tangu alipopona majeraha yake, alikiri kuwa hakuwa kwenye ubora  wake.

Akizungumza na Nipashe kutoka Mwanza, Tambwe, alisema Mbao waliwapania na kuchezea soka la kibabe hivyo kufanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0.

Pia alisema kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wao kwenye nafasi za kiungo, ulinzi na ushambuliaji kuliwapa nafasi Mbao kutamba kwenye mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

"Tumeumia kupoteza mechi... mchezo ulikuwa mgumu na wenzetu ni kama walitukamia na tukashindwa kucheza soka letu," alisema Tambwe.

Aidha, alisema hakuonyesha makeke yake kutokana na kuwa huo ulikuwa mchezo wake wa pili na wa kwanza kwenye ligi tangu alipotoka kuuguza majeraha.

"Makali yangu yatarudi kwenye mechi zinazokuja, tutajipanga kwa michezo mingine baada ya kumalizika kwa Mapinduzi Cup," alisema Tambwe.

Tambwe aliwekwa kwenye ulinzi mkali na beki kisiki wa Mbao, Yusuph Ndikumana na kushindwa kuonyesha makeke yake hasa kwenye ufungaji.

Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, licha ya kipigo hicho inaendelea kushika nafasi ya tatu ikiwa na pointi zake 21, tano nyuma ya vinara Simba na Azam zilizopo kileleni mwa ligi hiyo zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

 

Habari Kubwa