Simba yafuata dawa Sauzi leo

16Jul 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Simba yafuata dawa Sauzi leo
  • ***Ni kwa ajili ya kuiua Yanga ngao ya jamii, straika Mghana kunogesha mambo Sauzi...

MABINGWA wa Kombe la FA, Simba wamefuata dawa Afrika Kusini ya kuiua Yanga katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayopigwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Simba na Yanga zinatarajiwa kumenyana katika mechi hiyo itakayokuwa maalum kwa ajili ya ufunguzi wa msimu wa 2017/18.

Kundi la kwanza la wachezaji wa Simba linatarajia kuondoka nchini leo kwenda Afrika Kusini kujiandaa na mechi hiyo pamoja na msimu mpya ambao utaanza kurindima kuanzia Agosti 26, mwaka huu.

Imeelezwa kuwa kundi hilo la kwanza linatarajiwa kuongozwa na nahodha wa timu hiyo, Jonas Mkude, ambaye juzi aliripoti katika mazoezi na wachezaji wenzake.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa kundi la pili litahusisha wachezaji wa kigeni ambao walikuwa bado hawajaripoti kwenye mazoezi na huenda wakajiunga na wenzao moja kwa moja huko Afrika Kusini.

"Hapa nawazungumzia Okwi (Emmanuel), straika Mghana (Nicholas Gyan) yeye kama taratibu za kuja nchini leo (jana) zitakwama, tayari tumeshaandaa utaratibu mwingine wa kwenda Afrika Kusini akitokea kwao na jembe letu lingine (jina tunalihifadhi) lenyewe linasubiri tu mkataba wake na klabu yake ya zamani umalizike," kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilisema kuwa klabu inatarajia kumpa mkataba wa miaka miwili straika huyo ambaye msimu uliopita alitangazwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Ghana.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa kundi la tatu litakuwa ni la wachezaji walioko katika timu ya Taifa (Taifa Stars) ambao wataenda Afrika Kusini baada ya kumaliza mchezo wa marudiano dhidi ya Rwanda.

Ikiwa Afrika Kusini, Simba inayofundishwa na Mcameroon Joseph Omog, itacheza mechi za kirafiki kati ya mbili na tatu kabla ya kurejea nchini kutambulisha kikosi chake kipya kwenye Tamasha la Simba Day litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu.

Wakati huo huo Simba inasubiri barua rasmi kutoka kwa klabu moja ya Serbia ambayo imeonyesha nia ya kumsajili beki wa kati wa timu hiyo Mganda Juuko Murshid.

Beki huyo wa timu ya Taifa ya Uganda (Uganda Cranes) ana mkataba na Simba utakaomalizika Desemba mwaka huu.

Simba ambayo itaanza kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani, pia itatumia kambi hiyo ya Afrika Kusini kujiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika hapo mwakani.

Habari Kubwa