Simba kupokonywa pointi tatu za Kagera

16Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Simba kupokonywa pointi tatu za Kagera
  • ***Malinzi azishikilia kwanza, yashindwa kuvunja rekodi ya Toto Kirumba...

WAKATI Simba ikibanwa na Toto Africans jana kwa kulazimishwa sare tasa katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, vinara hao wa ligi kuna hatihati ya kupokonywa tena pointi tatu za Kagera Sugar-

SIMBA VS KAGERA SUGAR

walizozawadiwa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72.

Ikiwa ni siku tatu baada ya Kamati ya Saa 72 kuipa Simba pointi tatu kufuatia kukata rufani dhidi ya Kagera Sugar, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amezishikilia pointi hizo kupitia kamati ya shirikisho hilo.

Kwa mujibu wa taaifa iliyotolewa jana na TFF, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatarajiwa kukutana Jumanne Aprili 18, 2017 kwa lengo la kupitia uamuzi uliofanywa na Kamati ya Saa 72.

Taarifa hiyo, ilieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ina mamlaka ya kutafsiri sheria na kanuni za mpira wa miguu nchini kama ilivyoainishwa kwenye katiba na sehemu ya utangulizi ya kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kamati hiyo inakutana kutokana na ombi la timu ya Kagera Sugar ambayo imeomba kupitiwa upya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Saa 72 ambayo kwa mujibu wa kanuni, ilitoa matokeo mapya ya mchezo kati ya timu hiyo na Simba uliofanyika Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Katika mchezo huo, Kagera Sugar ilishinda mabao 2-1, lakini Simba ilikata rufaa ikidai kuwa Kagera Sugar ilivunja kanuni ya 37 (4) ya Ligi Kuu kwa kumchezesha mchezaji Fakhi Mohammed ambaye alidaiwa kuwa na kadi tatu za njano katika mechi tofauti za Ligi Kuu. Hivyo, ikaadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 37 (37) ambayo ilitoa pointi tatu na magoli matatu kwa Simba.

Hata hivyo, Malinzi jana alikataa kuzungumza lolote kuhusiana na taarifa hizo.
Katika taarifa ya wito iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Ahmad Yahaya, kikao hicho pia kitawahusisha waamuzi, maofisa wa bodi hiyo na kamishna wa mchezo huo.

"Kila mmoja atatakiwa kufika na nyaraka muhimu kuhusiana na mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya African Lyon," ilisema sehemu ya barua hiyo.

Simba yabanwa na Toto

Katika mchezo wa jana Simba ilibanwa na Toto Africans na kuondoka na pointi moja hivyo kwa jumla Kanda ya Ziwa kuzoa jumla ya pointi saba tu katika mechi tatu.

Sare hiyo imeendeleza rekodi mbaya ya Simba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya Toto, kwani haijawahi kuishinda kwa miaka saba sasa.

Mara ya mwisho Simba kuifunga Toto kwenye uwanja huo ni Januari 31, 2010, Ligi Kuu msimu wa 2009/10 iliposhinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Mussa Hassan Mgosi na Ramadhani Chombo 'Redondo.'

Kwenye mechi ya jana, Simba ilionekana kuwa makini kwenye safu ya ulinzi, lakini tatizo lilikuwa kwenye safu ya ushambuliaji, wachezaji wake, Fredrick Blagnon na Laudit Mavugo, hata Ibrahim Ajibu aliyeingia kipindi cha pili hawakuwa makini walipokuwa wakilikaribia lango la wapinzani wao.

Shiza Kichuya alishindwa kuitendea haki krosi ya Janvier Bokungu dakika ya pili na mpira huo ukatoka nje.

Waziri Junior, aliyewaliza Simba mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita kwenye Uwanja wa Taifa, alitumia makosa ya walinzi wa Simba kuzubaa, akaachia shuti kali lililotoka nje ya lango.

Toto ilikosa bao lingine dakika ya 19, baada ya Juvenary Pastory alipounganisha krosi, lakini mpira ukapita juu la lango la Simba.

Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 62, huku Toto ikiwa imefikisha pointi 25.

Habari Kubwa