Serengeti Boys: Ushindi kila mechi Gabon

16Apr 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Serengeti Boys: Ushindi kila mechi Gabon

WAKATI Mei 15, mwaka huu Serengeti Boys ikitarajia kuanza kampeni yake ya kuwania taji la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji chini ya umri wa miaka 17, dhidi ya Ethiopia, lengo lao ni kushinda kila mechi, imeelezwa.

Katika michuano hiyo itakayofanyika Gabon kuanzia Mei 14, Serengeti Boys ipo Kundi B sambamba na Niger, Angola na Ethiopia ambayo imepata nafasi hiyo baada ya Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf), kuiengua Mali kutokana na serikali ya nchi hiyo kuingilia masuala ya soka.

Kocha wa Serengeti Boys, Bakari Shime, jana aliliambia Nipashe kwa njia ya simu kutoka Morocco walikoweka kambi kuwa, kikosi chake kimehamasika na kuimarika vema, hivyo hahofii timu yoyote watakayokutana nayo katika michuano hiyo.

"Lengo letu ni kushinda mechi zote kabla ya kutwaa ubingwa, vijana wapo vizuri na tunaendelea kujipanga," alisema Shime ambaye ameiongoza Serengeti Boys kwa mafanikio makubwa hadi kufanikiwa kufuzu michuano hiyo.

Shime alisema timu zote ni ngumu katika michuano hiyo, na kwamba kutokana na kulitambua hilo wanaendelea kujipanga ili kupata ushindi katika kila mchezo na kutimiza malengo yao.

Habari Kubwa