Samatta apigiwa debe bungeni

23May 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Samatta apigiwa debe bungeni

MBUNGE wa Viti Maalum (CCM), Amina Mollel, ameitaka serikali kutambua mchango wa Mbwana Samatta kutokana na mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kuwakilisha vema Tanzania kimataifa.

Mbwana ambaye ni mshambuliaji wa timu ya Genk ya Ubelgiji ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa upande wa wachezaji wanaotoka barani Afrika.

Akiomba mwongozo wa Spika, Mollel alisema serikali ipo kimya licha ya Mbwana kuiwakilisha vema Tanzania kimataifa. 

“Samatta anayecheza soka la kulipwa nchini Ubelgiji ameiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa na ameongoza ligi hiyo kwa kufunga mabao 23 kutokana na kazi nzuri aliyoifanya Mtanzania mwenzetu na tumeona wenzake na hasa wenyeji wakishangilia kwa kutumia bendera ya Tanzania ni dhahiri kabisa ameitangaza vema nchi yetu,” alisema.

Mollel aliomba kupata kauli ya serikali kuhusiana na jambo hilo ili kutoa motisha kwa Watanzania wengine.

“Kwenye mtandao ameandikwa kwamba ni Mkenya ninaomba kauli ya serikali ili wengine waache kudandia dandia,” alisisitiza.

Akijibu mwongozo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema watawasiliana na serikali namna ya kushughulika na jambo hilo wakati mwafaka.