Omog: Ni fainali leo

08Jan 2017
Mahmoud Zubeiry
Nipashe Jumapili
Omog: Ni fainali leo
  • ***Kundi lawa gumu, ahofia muziki wa Jang'ombe Boys ulioiua URA waliyotoka nayo sare...

WAKATI hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi ikitarajiwa kuhitimishwa leo kwa michezo miwili ya Kundi A, ambayo itaamua timu za kwenda nusu fainali, kocha wa Simba Mcameroon Joseph Omog amesema leo ni kama fainali.

Hadi sasa hakuna timu yenye uhakika wa nusu fainali katika kundi hilo, ikiwa URA inaweza kufikisha pointi saba za Simba na Jang’ombe Boys wanaweza kumaliza na pointi tisa.

Simba itacheza mechi ya kwanza leo dhidi ya Jang'ombe Boys kuanzia saa 10:00 jioni, wakati mabingwa watetezi, URA kutoka Uganda, wataingia katika mchezo wa pili dhidi ya Taifa Jang'ombe kuanzia saa 2:30 usiku.

Japokuwa inaongoza Kundi A kwa sasa, lakini Simba inaweza kujikuta inafungasha virago kurejea Dar es Salaam iwapo tu itafungwa leo.

Ushindi utawafanya wapinzani wao wafikishe pointi tisa na matokeo yoyote ya mchezo wa usiku yasiweze kuinusuru Simba kubaki kwenye mashindano.

Mechi ya usiku ikiisha kwa sare, Taifa itafikisha pointi saba, hivyo timu ya kuungana nayo itatazamwa kwa wastani wa mabao kwa kuwa hata URA wakishinda nao, watafikisha pointi saba.

Ni mbaya zaidi ikiwa Simba itapoteza mechi kwa Jang’ombe Boys na Taifa Jang’ombe ikashinda pia. Hapo ni wazi Simba wanaingia katika mchezo mgumu leo, ambao watahitaji japo sare ili kuwapunguza Jang’ombe Boys.

Tayari Omog ameshasema kwamba anatarajia upinzani mkali leo kutoka kwa Jang’ombe Boys.

Omog alisema Jang’ombe Boys ni timu nzuri na ilidhihirisha hilo baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, URA kwa mabao 2-1, hivyo hata mbele ya Simba watakuwa tishio tu.

Kwa sababu hiyo, Omog amesema amewandaa vizuri vijana wake kwenda kucheza kwa tahadhari ili kuepuka kuingia kwenye mitego ya Jang’ombe Boys.

“Utakuwa mchezo mgumu. Hiyo timu (Jang’ombe Boys) imewafunga wanaoshikilia kombe, imefunga timu nzuri ambayo sisi tumetoka nayo sare, kwa hiyo tunauelekea mchezo mgumu na tutacheza kwa tahadhari tupate matokeo mazuri twende nusu fainali,”alisema Omog.

Simba inaongoza Kundi A kwa pointi zake saba, baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Taifa Jang’ombe, 1-0 dhidi ya KVZ na sare ya 0-0 na URA. Jang’ombe Boys wanafuatia kwa pointi zao sita, mbele ya URA yenye pointi nne na Taifa pointi tatu.

Nusu fainali inatarajiwa kuchezwa Januari 10 na fainali Januari 13, mwaka mwaka huu.

Habari Kubwa