Okwi, Niyonzima  kuikosa Ndanda

28Dec 2017
Faustine Feliciane
Nipashe
Okwi, Niyonzima  kuikosa Ndanda

KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Masoud Djuma, amesema licha ya kutokuwa na baadhi ya nyota wake, wanaenda Mtwara kupambana kwa ajili ya ushindi.

Simba, ambayo wiki iliyopita iliondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), huku ikishuhudia kocha wake, Joseph Omog, akitimuliwa, leo inaifuata Ndanda FC mjini Mtwara kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu utakaochezwa Jumamosi.

Vinara hao wa Ligi Kuu wanaodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, watakosa huduma ya nyota wao wa kigeni, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima ambao wametoka kwenye majeraha na kwa sasa wameanza mazoezi mepesi.

Djuma, aliiambia Nipashe kuwa, mchezo huo ni muhimu zaidi kwao ili kuondoa machungu kwa mashabiki wao ya kuondolewa kwenye michuano ya FA.

“Hatutarajii mchezo mwepesi kwa sababu hata wao watakuwa wamejiandaa kutukabili, kikubwa ni lazima tukapambane bila kuangalia nani atakuwapo na nani hatokuwapo kwenye kikosi,” alisema Djuma.Alisema wanakwenda kuvaana na wapinzani wao hao (Ndanda FC) kwa tahadhari na amekiandaa kikosi kucheza soka la kasi.

“Mashabiki na hata wachezaji na benchi la ufundi bado tunakumbukumbu ya kuondolewa kwenye FA, lakini hilo hatupaswi kuliweka akilini tukiwa tunaelekea kuvaana na Ndanda, kwetu iwe kama chachu ya kuhakikisha tunapata ushindi,” aliongezea kusema Djuma.

Habari Kubwa