Mwakyembe kubariki Heart Marathon

21Apr 2017
Faraja Ezra
Nipashe
Mwakyembe kubariki Heart Marathon

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mbio za Heart Marathon zinazotarajiwa kufanyika Aprili 26 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe.

Mbio hizo pia zinatarajia kuhamasisha wadau wa michezo kushiriki katika zoezi la upimaji wa afya lengo likiwa ni kupunguza magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza jana kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), Rais wa Kituo cha Magonjwa ya Moyo, Omary Chillo, alisema kuwa watu zaidi ya 2,000 wanatarajia kushiriki mbio hizo.

Chillo alisema katika mashindano hayo washiriki watachuana katika mbio za kilomita 21.1 , kilomita tano wakati watoto chini ya umri wa miaka 12 watashiriki katika umbali wa mita 700.

Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Tanzania (RT), Ombeni Zavala, aliwataka wanariadha kutoka ndani na nje ya Dar es Salaam kujitokeza kushiriki mbio hizi kwa sababu ni sehemu nyingine ya kukuza vipaji vyao na kujiweka tayari na mashindano ya kitaifa na kimataifa.

Zavala alisema kuwa pia washiriki watapata nafasi ya kufanya vipimo vya magonjwa mengine kama shinikizo la damu, sukari, saratani pamoja na ushauri kutoka kwa madaktari wazoefu.

Alisema zawadi ya mshindi kwa upande wa wanaume na wanawake kila mmoja atajinyakulia Sh. 500,000.

Habari Kubwa