Msuva hatihati kuivaa Amavubi

17Jul 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Msuva hatihati kuivaa Amavubi

MSHAMBULIAJI wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars), Simon Msuva, yuko katika hatihati ya kwenda Kigali katika mchezo wa marudiano dhidi ya wenzao wa Rwanda utakaopigwa Jumapili jijini Kigali, imefahamika.

Katika mechi ya kwanza ya kuwania kufuzu fainali ya michuano ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Soka la Ndani (CHAN), iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, Taifa Stars na Amavubi zilitoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini hapa, Msuva alisema anatarajia kupata visa ya kwenda Morocco kati ya leo na kesho ili kwenda kukamilisha taratibu za usajili na klabu yake mpya ya Difaa El Jadida.

Msuva alisema anaamini akifika huko atakamilisha mchakato huo wa usajili na kuanza maisha mapya kucheza soka la kulipwa.

"Sina hakika kama nitaweza kwenda Kigali katika mechi ya marudiano maana kati ya kesho (Jumatatu) na Jumanne, visa yangu inaweza kutoka kwa ajili ya kwenda Morocco, itakavyokuwa ndio mipango ya safari yangu itaanza rasmi," alisema Msuva.

Aliongeza kuwa anashukuru viongozi wa Yanga kwa kufanikisha mchakato wake wa uhamisho na akiwa huko Morocco anaahidi kupeperusha vyema Bendera ya Tanzania ili kutoa nafasi ya wachezaji wengine wa hapa nchini kutangaza vipaji vyao na hatimaye kupata timu nje ya nchi.

"Najua ninakwenda huko kujitengenezea maisha yangu, sitafanya mchezo, nitacheza soka la juu ili kuzifutia klabu za Ulaya, ile ni timu kubwa iko katika nafasi ya pili, ni daraja la kusonga mbele," Msuva aliongeza.

Alisema anafurahi akiwa Morocco hatakuwa mpweke kwa kuwa atakuwa na mchezaji mwingine wa Tanzania, Ramadhani Singano.

Aliweka wazi kuwa mapenzi yake awali ilikuwa ni kwenda kucheza soka katika klabu ya Bid Vest ya Afrika Kusini, lakini usajili wake ulishindikana kukamilika kutokana na Yanga kuhitaji dau kubwa ili kuvunja mkataba wake.

Habari Kubwa