Mbao yatoa  neno Yanga

31Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe Jumapili
Mbao yatoa  neno Yanga

Kocha Mkuu wa Mbao FC, Etienne Ndayiragije, ametabiri mechi ya leo dhidi ya Yanga kuwa ngumu kwa sababu anaamini wapinzani wao hao watakuwa  wamejiandaa vema kutokana na kupoteza mechi zote ambazo  wamecheza na timu yake kwenye Uwanja wa CCM Kirumba,  Mwanza.

Kocha Mkuu wa Mbao FC, Etienne Ndayiragije.

Mechi hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuanzia majira ya saa 10:00 jioni, itabidi Yanga ishuke dimbani kwa tahadhari kutokana na kwamba hupata wakati mgumu inapocheza na timu hiyo uwanjani hapo.

Yanga haijawahi kuifunga Mbao kwenye uwanja huo, licha ya  kukutana mara mbili.

Mara ya kwanza ilikuwa ni kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe  la FA mwaka jana, Mbao ikaichapa Yanga bao 1-0, lakini pia  kwenye mechi ya Ligi Kuu, pia Yanga ililala kwa bao 1-0 dimbani hapo.

Akizungumza na Nipashe jana kuelekea mechi hiyo ya leo, Ndayiragije alisema kwa upande wake hana wasiwasi sana kutokana na jinsi alivyowaandaa vijana wake.

"Huwa nafurahishwa sana na vijana wangu kwa jinsi  wanavyopambana na kujituma, hasa wakicheza na timu hizi  kubwa," alisema kocha huyo.

Ndayiragije, kocha ambaye anasifika kufundisha soka la nguvu, alisema kwa upande wake anahitaji ushindi kwenye mechi hiyo,  ingawa anakiri kuwa itakuwa ngumu.

Yanga itawakosa mastraika wake tegemeo wawili ambao ni Ibrahim Ajibu anayedaiwa kuwa na kadi tatu za njano, lakini pia Obrey Chirwa ambaye amerejea nchini kwao Zambia na taarifa za ndani zinadai kuwa anaendelea na kilimo cha mahindi wakati huu ikielezwa kuwa ana mgomo wa kichinichini kushinikiza kulipwa pesa  zake.

Hata hivyo, Yanga inaweza kunufaika na kurejea kwa straika wake hatari Amissi Tambwe ambaye alikuwa majeruhi kwa muda mrefu,  huku akifunga bao kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Reha FC, lakini Mbao itakuwa ikimtegemea straika wao, Habib Haji  ambaye ana mabao matano kwenye Ligi Kuu, pia matano kwenye  Kombe la FA.

Yanga ina pointi 21 kwa mechi 11 ambazo imecheza huku Mbao FC  ikiwa na pointi 11.

 

Habari Kubwa