Mayanga: Stars inaweza kuichapa Amavubi kwao

17Jul 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe
Mayanga: Stars inaweza kuichapa Amavubi kwao

KOCHA wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars), Salum Mayanga, amesema timu yake bado ina nafasi ya kusonga mbele katika michuano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Wachezaji wa Ndani (CHAN), licha ya kuanza kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Rwanda hapo juzi.

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars), Salum Mayanga.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanga alisema anaamini wachezaji wake wanaweza kupambana na kupata ushindi ugenini licha ya kushindwa kufanya hivyo hapa nyumbani.

Mayanga alikiri kuwa matokeo ya sare hayakuwa mazuri, lakini bao la mapema walilofungwa liliwavuruga na kuwaondoa mchezoni.

"Jukumu letu sasa ni kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa kwanza, lilitufanya tusiwe na utulivu na kushindwa kutawala mchezo, tutatumia muda huu wa wiki moja kusahihisha makosa yote," alisema Mayanga.

Kocha huyo aliongeza kuwa jana aliwapa mapumziko wachezaji wake na leo wataanza tena kujifua kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano utakaopigwa Jumapili Julai 23, mwaka huu jijini Kigali.

Naye Kocha Msaidizi wa Amavubi, Vincent Mashami, aliwapongeza wachezaji wa timu zote mbili kwa matokeo waliyopata katika mchezo huo ambao ulikuwa ni mgumu na wenye ushindani.

"Kazi bado haijamalizika, ila hawa marefa sijui wametoka nchi gani, maana wanaharibu mpira na tukienda katika mashindano ya kimataifa tunashindwa kufanya vizuri, tunaijua Tanzania na wachezaji kama Msuva (Simon) wanauzoefu ambao wanaweza kubadilisha matokeo," alisema Mashami.

Tayari kikosi cha Amavubi kimesharejea kwao kuendelea na maandalizi ya mchezo wa marudiano.

Habari Kubwa