Mambo manne yamleta Rais Fifa

03Jan 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Mambo manne yamleta Rais Fifa
  • ***Kutua rasmi nchini mwezi ujao, usajili pia kujadiliwa kufuatia...

FURSA ya kibiashara kwenye soka, usalama wa nchi na ufanisi wa kozi mbalimbali zinazosimamiwa na Shirikisho la Soka duniani (Fifa), ni baadhi ya sababu zinazomfanya Rais wa Shirikisho hilo, Gianni Infantino, kupanga safari ya kuja nchini.

Rais wa Shirikisho la fifa, Gianni Infantino.

Rais huyo wa Fifa anatarajiwa kuja nchini Februari 21, mwaka huu kwa ajili ya kuendesha mkutano mkuu wa Kanda wa Fifa uliopangwa kufanyika Februari 22 jijini Dar es Salaam.

Mbali na Infatino, pia Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, Ahmad Ahmad, na makamu wake Kwesi Nyantakyi, nao watatua nchini kuhudhuria mkutano huo.

Mkutano huo utakaofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, utashirikisha nchi 19.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, aliliambia Nipashe jana kuwa mkutano huo utahudhuriwa na Marais na Makatibu wa mashirikisho ya soka kutoka katika nchi hizo 19 shiriki.

“Mkutano utafanyika Februari 22 na utamalizika kesho yake, huu ni ugeni mzito katika soka letu,” alisema Lucas huku akifafanua.

“Tutaanza kuwapokea wageni kuanzia Februari 20 kabla ya kumpokea Rais Infatino.”

Imefahamika kuwa Fifa mbali na kuvutiwa na mambo hayo, pia imekuwa na imani kubwa na uongozi mpya wa TFF ambao kwa sasa upo chini ya Rais Wallace Karia.

Lakini pia, TFF katika uchaguzi wa rais wa Fifa wa mwaka 2016, ambao ulimuweka madarakani Infatino, ilikuwa ikimuunga mkono Rais huyo mwenye uraia wa Uswisi na Italia ambaye alipata kura 115.

Wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ni pamoja na Sheikh Salman Bin Ebrahim Al Khalifa, ambaye alipata kura 88, Prince Ali Bin Al Hussein aliyeambulia kura 4 na Jerome Champagne (hakupata kura).

Ajenda kubwa katika mkutano huo wa Kanda zimetajwa kuwa ni utoaji wa fedha za Fifa kwa ajili ya maendeleo ya soka, changamoto za usajili kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System- TMS), soka la vijana na wanawake na mambo mengine muhimu katika soka.

Nchi 19 zitakazoshiriki mkutano huo mbali na mwenyeji Tanzania ni Algeria, Mali, Morocco, Burkinafaso, Angola, Niger, Bahrain, Palestina na Saud Arabia.

Zingine ni Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ivory Coast, Tunisia, Bermuda, Monserrat, St Lucia, Visiwa vya US Virgin, Maldives na  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Habari Kubwa