Makambo alinda heshima Yanga

23May 2019
Adam Fungamwango
DAR
Nipashe
Makambo alinda heshima Yanga

Yanga jana iliwafurahisha mashabiki wake wachache waliojitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, baada ya kuichapa Mbeya City bao 1-0 na kufikisha pointi 86 hivyo kuendelea kupunguza wigo wa pointi dhidi ya mabingwa Simba wenye alama 91 na mechi mbili mkononi.

Heritier Makambo.

Alikuwa ni Mkongomani Heritier Makambo aliyelinda heshima ya Yanga kwa kufunga bao dakika ya 25 akiunganishwa kwa kichwa, mpira wa adhabu uliopigwa na Mwinyi Haji na kufikisha jumla ya mabao 17 sawa na John Bocco wa Simba, ikiwa ni sita nyuma ya kinara Meddie Kagere wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Kabla ya hapo, Makambo alikosa bao akiwa peke yake, alipopigwa kichwa mpira wa krosi, lakini uligonga mwamba wa juu na kuokolewa na walinzi wa Mbeya City.

Makambo, ambaye hivi karibuni aliteka vyombo vya habari kutokana na kuonekana akisaini mkataba wa kuichezea Klabu ya Horoya ya nchini Guinea, alijitahidi kutaka kufunga mabao zaidi ili kuendelea kumfukuza Kagere mwenye mabao 23, lakini mashuti yake hayakuwa na macho.

Kipindi cha pili Mbeya City ilikuja juu kutaka kusawazisha bao, ikiwatumia mastraika wake tegemeo, Idd Suleiman 'Nado', Victor Angaya, wakisaidiwa na winga wao machachari aliyeingia kipindi cha pili, Peter Mapunda, lakini mabeki wa Yanga wakiongozwa na Kelvin Yondani walisimama imara kuondoa hatari zote golini.

Yanga iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, imebakisha mechi moja tu, dhidi ya Azam FC, itakayochezwa Mei 28, siku ya funga msimu wa 2018/19 Ligi Kuu Tanzania Bara.

Habari Kubwa