Kiyombo alijitabiria kuiua Yanga

02Jan 2018
Faustine Feliciane
Nipashe
Kiyombo alijitabiria kuiua Yanga

 MSHAMBULIAJI nyota wa Mbao FC, Habib Kiyombo, amesema kuwa anashukuru kutimiza ahadi aliyoitoa kabla ya mchezo wa juzi dhidi ya Yanga kuwa atawafunga mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

 MSHAMBULIAJI nyota wa Mbao FC, Habib Kiyombo.

Kiyombo juzi alikuwa mwiba mkali kwa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, wakati wa mchezo wao wa Ligi Kuu uliopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo alifunga mabao yote mawili wakati wakishinda 2-0.

Akizungumza na Nipashe jana, Kiyombo alisema kuwa kabla ya mchezo huo aliahidi kuwa lazima atawatungua wababe hao wa     Ligi Kuu kitu ambacho amekifanikisha.

"Niliahidi, na namshukuru Mungu nimetimiza ahadi yangu, nimefurahi kuona tumeibuka na ushindi huu mzuri dhidi ya timu kubwa kama Yanga, lakini furaha zaidi ni kuona mabao hayo nimeyafunga mimi," alisema Kiyombo.

Alisema kuwa timu yake ilipata ushindi kutokana na juhudi za wachezaji pamoja na kufuata maelekezo ya kocha wao.

"Tulichokifanya ni kujituma na mwalimu ambaye alikuwa nje alikuwa anaona mapungufu ya wapinzani wetu na kutupa maelekezo ya nini cha kufanya na kweli tulifuata na kuibuka na ushindi," alisema mshambuliaji huyo.

Aidha, mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa anashika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji msimu huu, alisema atahakikisha anafunga katika kila mchezo pindi anapopata nafasi.

"Naomba Mungu niendelee kupata nafasi na kuendelea kuaminiwa na kocha, nitaendelea kujituma na kufanya vizuri," alisema mshambuliaji huyo.

Ushindi walioupata Mbao juzi ni wa tatu mfululizo dhidi ya Yanga katika michezo mitatu waliyokutana nayo tangu wamepanda Ligi Kuu Bara.

Habari Kubwa