Kipa Stars akabidhiwa tuzo ya Cosafa Mwanza

16Jul 2017
Somoe Ng'itu
Nipashe Jumapili
Kipa Stars akabidhiwa tuzo ya Cosafa Mwanza

KIPA chaguo la pili wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Said Mohamed, jana alikabidhiwa tuzo yake ya mlinda mlango bora wa michuano ya Kombe la Cosafa aliyoshinda kwenye kinyang'anyiro hicho kilichomalizika hivi karibuni huko Afrika Kusini.

Mohamed alipata tuzo hiyo baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu ambayo Taifa Stars iliikabili Lesotho na ndani ya dakika 90 za kawaida, timu hizo zilitoka suluhu na Tanzania ikaibuka kidedea kwa kupata penalti 4-2.

Kipa huyo wa Mtibwa Sugar alipangua penalti moja huku pia Kamati ya Ufundi ya mashindano ya Cosafa ikimuelezea kuwa hakuwa na makosa mengi ya kiufundi na akiwa amecheza mchezo huo mmoja tu kwa Taifa Stars.

Kaimu Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ndiye alimkabidhi Mohamed tuzo hiyo aliyoipokea huko Afrika Kusini katika tukio fupi lililofanyika kwenye Hoteli ya Isamilo jijini hapa.

Baada ya kupokea tuzo hiyo Mohamed alisema imemuongezea uwezo wa kujiamini na amejipanga kuendelea kujituma kila atakapopata nafasi katika klabu au timu ya Taifa.

"Uvumilivu na nidhamu ni moja ya vitu ninavyojivunia katika kazi yangu, naipenda pia kazi hii na nitafanya kila ninaloweza ili kuisadia timu kupata ushindi ninapokuwa langoni," alisema kipa huyo ambaye aliwahi pia kuichezea Yanga.

Mohamed ni mmoja kati ya makipa watatu wa Taifa Stars, ambayo inasaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ambazo zitafanyika nchini Kenya hapo mwakani.

Habari Kubwa