DTB yaifikiria Ligi Kuu Bara

23May 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
DTB yaifikiria Ligi Kuu Bara

TIMU ya Diamond Trust Tanzania (DTB FC) ya jijini Dar es Salaam imefanikiwa kufuzu kucheza Ligi Daraja la Pili Ngazi ya Taifa msimu ujao wa mwaka 2019/2020 baada ya kushika nafasi ya pili katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa iliyomalizika mwishoni mwa wiki mkoani Simiyu.

Wachezaji wa timu ya soka ya DTB wakishangilia baada ya kufanikiwa kufuzu kucheza Ligi Daraja la Pili ngazi ya taifa msimu wa 2019/2020, kufuatia kuibuka washindi wa pili katika Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) 2018/2019 mkoani Simiyu. MPIGAPICHA WETU

DTB FC ilipoteza mchezo wa fainali dhidi ya Pan African uliomalizika kwa ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya klabu hiyo kongwe ya jijini pia.

Ndani ya dakika 90 timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na zilipoongezwa dakika 30 matokeo yalikuwa ni sare ya 2-2 huku mabao yote mawili ya DTB yakifungwa na Hussen Juma, hivyo hatua ya penalti kuchukua nafasi yake.

Fainali za Ligi ya Mabingwa wa Mikoa maarufu RCL iliochezwa Simiyu ilikutanisha timu nane zilizopangwa katika makundi mawili ambapo Kundi A lilikuwa na DTB, Isanga Rangers kutoka Mbeya, Top Boys (Ruvuma) na wenyeji Bariadi United.

Kundi B liliundwa na Pan African, Mbuni FC (Arusha), Mji Mpwapwa (Dodoma) na Mkurugenzi FC kutoka mkoani Katavi.

Akizungumza na gazeti hili, Kocha Mkuu na Meneja wa DTB FC, Michael Lugalela, alisema timu yake ilipambana hadi kufika hatua hiyo na kuweka wazi mashindano hayo yalikuwa na ushindani sana.

“Matazamio yetu ni kufika Ligi Kuu Tanzania Bara, japo tunajua ni kazi ngumu, lakini inawezekana kama tutajiandaa vema kwa kufanya mazoezi na kujituma, pia tukipata ushirikiano kutoka kwa uongozi wa benki tulianza safari hii katika ngazi ya chini sana ya Daraja la Tatu na macho yetu yanaitazama Ligi Kuu ya Tanzania. Itachukua muda kidogo, lakini tumeanza hatua ya kwanza," alisema kocha huyo.

Habari Kubwa