Dida: Hatuna bahati na penalti

12Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Dida: Hatuna bahati na penalti

GOLIKIPA namba moja wa Yanga, Deogratius Munishi 'Dida' amesema timu yake imekosa bahati kwenye upigaji wa penalti licha ya kufanyia mzoezi mara kwa mara.

Deogratius Munishi 'Dida' .

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Dida, alisema matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wa juzi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Simba yanatokana na kukosa bahati, lakini walicheza vizuri muda wote wa mchezo.

"Mechi za Simba na Yanga zinapresha kubwa... tulicheza vizuri, lakini hatukuwa na bahati kwenye penalti na hili ni tatizo letu mara nyingi tunapofika hatua ya penalti," alisema Dida.

Aidha, golikipa huyo wa timu ya Taifa 'Taifa Stars', amewaomba radhi mashabiki wa timu hiyo kwa kuondolewa kwenye michuano hiyo hatua ya nusu fainali.

"Tunafahamu mashabiki wetu walikuwa na matumaini makubwa na sisi..., tunaomba radhi kwa kuondolewa hatua hii ya nusu fainali, lakini bado tupo kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na pia tupo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, tuna uwezo wa kufanya vizuri huko," alisema Dida.

Yanga iliondolewa juzi kwenye michuano hiyo na Simba baada ya kukubali kipigo cha penalti 4-2 baada ya kumaliza dakika 90 bila kufungana.

Dida na beki wa pembeni Haji Mwinyi walikosa penalti zao huku Simon Msuva na Thaban Kamusoko wakifunga kwa upande wao. Beki Method Mwanjali alikosa kwa upande wa Simba huku waliofunga penalti zao wakiwa ni Jonas Mkude, Daniel Agyei, Mudhamir Yassin pamoja na Javier Bukungu.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar, kipindi cha kwanza Yanga ilimiliki mpira kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Simba, wakati kipindi cha pili Simba ikimiliki kwa asilimia 54 dhidi ya 46 za Yanga.

Habari Kubwa