CCM yatenga Mil. 188/- Namfua

20Mar 2017
Jumbe Ismaily
Nipashe
CCM yatenga Mil. 188/- Namfua

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kinatarajia kutumia Sh. milioni 188 kwa ajili ya kufanya matengenezo kwenye Uwanja wa Namfua ili uweze kukidhi sifa na kutumika katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeelezwa.

Mwenyekiti wa ccm, Mkoa wa Singida, Martha Mlata.

Mwenyekiti wa chama hiko mkoani hapa, Martha Mlata alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa jumuiya za chama hicho baada ya kuukagua uwanja huo.

Tayari matengenezo ya kuweka udongo mpya na kuondoa ule wa zamani yameshaanza.

“Tumeshafanya makadirio ya kiasi cha fedha ambacho kinatarajia kutumika katika matengenezo ya uwanja wetu, hiyo itatokana na kupata au kutopata msaada kutoka kwa wahisani," alisema kiongozi huyo.

Mlata ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu mkoani hapa alisema kuwa kati ya fedha hizo zinazotarajiwa kutumika, Sh. milioni 10 zitaenda kununua majani maalumu yatakayopandwa kwenye uwanja huo.

Hata hivyo mwenyekiti huyo aliweka wazi sababu za chama hicho kuamua kuufanyia matengenezo uwanja wa michezo wa kumbukumbu ya Namfua inatokana na kutekeleza ilani ya uchaguzi wa CCM kuhusu kuendeleza michezo.

Naye msimamizi wa kazi hiyo, Saidi Ibrahim alibainisha kuwa kazi iliyopo kwa sasa ni kuongeza udongo utakaotumika kupandia majani baada ya kutoa changarawe iliyokuwa imewekwa katika siku za awali.

Singida inatarajia kushuhudia mechi za Ligi Kuu Bara baada ya timu yake ya Singida United kupanda daraja. Timu nyingine zilizokata tiketi ya kushiriki ligi hiyo msimu ujao ni pamoja na Njombe Mji na Lipuli.

Habari Kubwa