Bocco alinda  rekodi Simba

31Dec 2017
Adam Fungamwango
Nipashe Jumapili
Bocco alinda  rekodi Simba
  • ***Ni ya Wekundu wa Msimbazi kuendeleza vipigo kwa Ndanda...

MABAO mawili yaliyofungwa na mshambuliaji John Bocco, wakati wakishinda 2-0 dhidi ya Ndanda FC jana, yameirejesha Simba kileleni mwa Ligi Kuu Bara, baada ya Azam FC kuongoza kwa muda kuanzia juzi usiku.

Ushindi huo kwa Simba ni wa nne mfululizo kwenye Uwanja wa  Nangwanda Sijaona tangu timu hizo zilipoanza kukutana uwanjani hapo.

Pia ni ushindi wa saba mfululizo kwa Simba dhidi ya timu hiyo  kwenye viwanja vyote vya nyumbani na ugenini tangu timu hiyo  ipande daraja na kuanza kucheza Ligi Kuu, msimu wa 2014/15.

Kadhalika, ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa kocha Masudi Djuma kama Kocha  Mkuu, akikaimu nafasi ya Mcameroon Joseph Omog ambaye  alitimuliwa wiki iliyopita kufuatia timu hiyo kuong'olewa kwenye  michuano ya Kombe la FA dhidi ya timu ya Daraja la Pili, Green  Warriors.

Katika mechi hiyo ya jana, baada ya kosa kosa nyingi kipindi cha kwanza, Simba ilirejea  kipindi cha pili kwa nguvu na kucheza mpira wa kasi na  iliwachukua dakika saba tu kuandika bao la kwanza.

Bocco alifunga bao hilo dakika ya 52 kwa kichwa, akiunganisha  mpira wa kona uliopigwa na Shiza Kichuya ambaye alichezeshwa kama  beki wa kushoto kwenye mechi hiyo ya jana.

Dakika nne baadaye, Bocco, aliyesajiliwa msimu huu akitokea  Azam FC, alifunga bao la pili baada ya mabeki wa Ndanda kumsahau, huku wakiwa wamemkaba Mosses Kitandu  liyeonekana kuukimbiza mpira huo.

Hiyo ni baada ya mpira mrefu uliopigwa na Said Ndemla na  kuonekana kama unatoka, lakini aliudokoa na mpira ukajaa wavuni  na kumuacha kipa Jeremiah Kasubi asijue la kufanya.

Ndanda ilijitahidi kutaka kurudisha mabao hayo, huku mastraika  wake Mrisho Ngassa, Alex Sethi, Omari Mponda na Hemes Koja wakijitahidi kulitia msukosuko lango la Simba lililokuwa likilindwa na kipa Aishi Manula, Juuko Murshid, Paul Mukaba, Erasto Nyoni  na Yusuph Mlipili aliyeingia kipindi cha pili, lakini  hawakufanikiwa.

Kwa matokeo hayo, Simba inakaa kileleni ikiwa na pointi 26 sawa na Azam FC, lakini Wekundu wa Msimbazi hao wakiwa na tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa kufuatia Azam FC nayo juzi kushinda 3-0 dhidi ya Stand United.

Baada ya mechi ya leo kati ya Yanga na Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ligi hiyo itasimama tena kwa muda kupisha michuano ya Kombe  la Mapinduzi mjini Zanzibar.

Habari Kubwa