Aveva: Haki yetu itapatikana Fifa

20May 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Aveva: Haki yetu itapatikana Fifa

WAKATI Ligi Kuu Tanzania Bara inatarajia kumalizika leo, Klabu ya Simba rasmi imepeleka malalamiko yake katika Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ya kudai pointi tatu baada ya Kagera Sugar kumchezesha beki wake Mohammed Fakhi ambaye alikuwa na kadi tatu.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyofanyika Aprili 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba, wenyeji walipata ushindi wa mabao 2-1.

Baada ya mechi hiyo kufanyika, Simba iliwasilisha malalamiko katika Bodi ya Ligi Kuu na kupewa pointi tatu na mabao matatu lakini uamuzi huo utatenguliwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ndani ya muda mfupi.

Akizungumza na gazeti hili jana, Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema katika barua yao hiyo wameieleza Fifa wanataka haki itumike kwa kuzingatia kanuni za ligi baada ya Kagera Sugar kumtumia mchezahi huyo ambaye alikuwa na kadi tatu za njano.

Aveva alisema kuwa wameamua kulifikisha suala hilo Fifa baada ya kuona vyombo vya hapa nyumbani vimewanyima haki yao.

"Ni kweli tumeshatuma malalamiko yetu rasmi tangu juzi (Jumatano) kwa njia ya nukushi na barua pepe, tukiwa tumepeleka vielelezo vyote muhimu," Fakhi katika mechi hiyo.

Rais huyo aliongeza kuwa wameamua kuwasilisha shtaka hilo la kadi tatu za njano na wakiweka kiporo usajili wa Mbaraka Yusuph ili kuepuka kujichanganya na hapo baadaye watawasilisha pia suala hilo katika chombo hicho cha juu duniani.

"Tunaamini hatujachelewa hata kama ligi inamalizika kesho (leo), tutaiangalia hiyo hukumu ya Fifa na tusiporidhika nayo tutakwenda CAS (Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo," Aveva aliongeza.

Endapo Simba itashinda katika mchezo wake wa leo dhidi ya Mwadui FC utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa na kushinda malalamiko yake huku ikiwaombea Yanga kufungwa dhidi ya Mbao FC leo itafanikiwa kutwaa ubingwa huo walioukosa kwa muda mrefu.

Habari Kubwa