Arthur aanza kuwa  mtamu Azam FC

31Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Arthur aanza kuwa  mtamu Azam FC

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Mromania Aristica Cioaba, amepata fursa nzuri ya kushuhudia utamu wa mshambuliaji mpya, Mghana Bernard Arthur, wakati akiitumikia timu hiyo kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam juzi usiku na kuiwezesha kushinda 3-0 dhidi ya Stand United.

Bernard Arthur.

Cioaba, ambaye katika mechi hiyo alikuwa jukwaani akitumikia adhabu, alimshuhudia Arthur akiwa miongoni mwa wafungaji katika ushindi huo ambao ulizidi kuipaisha Azam kileleni kwa kufikisha pointi 26 baada ya mechi 12.

Katika mchezo huo, Azam ilianza kupata bao la kuongoza dakika ya 21, likifungwa na kiungo Salmin Hoza aliye katika msimu wake wa kwanza Chamazi kufuatia kusajiliwa na timu hiyo akitokea Mbao FC ya Mwanza.

Mfungaji huyo aliachia shuti la takriban umbali wa maguu 20 ya mtu mzima baada ya kutengewa pasi na kiungo wa ulinzi, Mcameroon Stepgan Mpondo.

Azam ambayo ilionekana kutawala dakika 45 za kipindi cha pili, ilifanya mabadiliko dakika ya 32 ikimtoa kinda Iddi Kipangwile na kumuingiza Arthur.

Kuingia kwa Arthur kuiifanya safu ya ushambuliaji kuongeza kasi, lakini umakini wa kipa wa Stand United, Frank Muwonge, uliwafanya Azam kukosa mabao.

Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi Emmanuel Mwandembwa kutoka Arusha, ilishuhudiwa Arthur akifumua shuti zuri lililokwenda nje sentimita chache baada ya pasi nzuri ya Mghana mwenzake, winga Enock Atta Agyei.

Dakika ya 64, Arthur alianza kuonyesha umuhimu wake wa kusajiliwa Azam baada ya kuitendea haki pasi ya Yahya Zayed kwa kumpiga chenga kipa, Muwonge kabla ya kuzamisha mpira kambani.

Bruce Kangwa aliiandikia Azam bao la tatu dakika ya 78, baada ya kuwapangua mabeki wa Stand United na kuingia ndani ya boksi kabla ya kufumua shuti lililompita kipa Muwonge.

Habari Kubwa