Alliance kutosajili wakongwe

08Mar 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Alliance kutosajili wakongwe

UONGOZI wa timu ya soka ya Alliance ambayo itacheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao umesema kuwa haitawapa nafasi ya kuwasajili wachezaji wakongwe katika kikosi chao kama klabu nyingine zinavyofanya mara zinapopanda daraja.

Mwenyekiti wa Alliance FC, James Bwire.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Alliance FC, James Bwire, alisema uongozi wa timu hiyo unawaamini wachezaji wake vijana ambao walipambana na kufanikisha kuipandisha timu na wanachohitaji ni kuongezewa mafunzo zaidi.

Bwire alisema kuwa wachezaji wao wameshapata uzoefu na kama wamefanikiwa kuhimili changamoto na ushindani ulioko katika Ligi Daraja la Kwanza, wanaamini pia watafanya hivyo kwenye Ligi Kuu.

Alisema kuwa wanajua ushindani watakaokutana nao na wamejipanga kuifanya Alliance isiwe "tawi" la klabu yoyote kati ya Simba na Yanga ambazo hugawa wapenzi mara wanapofika mikoani kucheza mechi zao za Ligi Kuu.

"Siamini katika wakongwe peke ndio wanaoweza kuisaidia timu kupambana, tumejipanga kuhakikisha tunakuwa timu ya mfano kwenye ligi kuu, hatuna jipya ila kila kitu tutafanya kwa kufuata taratibu ili mambo yetu yawe vizuri," alisema mwenyekiti huyo.

Aliongeza kuwa ili kupata wachezaji zaidi, wataendelea na programu ya kuendeleza wachezaji vijana kwa kuwaandaa wachezaji wa kuanzia umri chini ya miaka 12 hadi 17.

Mbali na Alliance, timu nyingine zilizopanda daraja ni pamoja na Coastal Union ya jijini Tanga na JKT Tanzania ya Dar es Salaam. 

Habari Kubwa