Zanzibar inahitaji polisi zaidi, siyo kufunga vituo

18Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Zanzibar inahitaji polisi zaidi, siyo kufunga vituo

KATIKA toleo letu la jana tulichapisha habari iliyoeleza kuwa Jeshi la Polisi Zanzibar limelazimika kufunga vituo vidogo katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, kutokana kukabiliwa na upungufu wa askari visiwani humo.

Kwa mujibu wa habari hiyo iliyotokana na mahojiano ya gazeti hili na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, vituo hivyo vimefungwa na sasa vitatumiwa na askari jamii katika kuimarisha ulinzi.

Kamishna Hamdan alisema baada ya vituo hivyo kufungwa, wananchi wanatakiwa kuripoti matatizo yao katika vituo vya polisi vya karibu yakiwamo makosa ya uhalifu yanayotokea katika maeneo yao.

Vile vile, alisema ulinzi shirikishi wa polisi jamii haujahamasishwa kwa kiwango kikubwa Zanzibar licha ya hatua mbalimbali za viongozi wa polisi wilaya na mkoa kuchukua hatua za kuhamasisha wananchi.

Pamoja na Jeshi la Polisi Zanzibar kuamua kufunga vituo vidogo kutokana na kutokuwa na askari wa kutosha, lakini uamuzi huo una athari zaidi kwa kuwa utasababisha kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu pamoja na kuongeza majalada ya kesi katika vituo vya polisi.

Ni kwa sababu vituo hivyo vitalazimika kuhudumia wananchi ambao walikuwa wanapata huduma katika vituo vidogo ambavyo vimeanza kufungwa.

Sote tunafahamu kuwa vituo vidogo haviwezi kutoa huduma kwa wananchi kama havina askari, hivyo hatua muhimu ya kuchukua ni kuongeza idadi ya askari Zanzibar ili vituo vyote vya polisi vikiwamo vidogo vitoe huduma kama ilivyokuwa awali.

Mbali na kufungwa kwa vituo vidogo Kamishna Hamdan ameelezea changamoto nyingine inayoikabili Zanzibar kuwa kutokuhamasika kwa ulinzi shirikishi ambao unashirikisha polisi na jamii.

Kwamba hali iko hivyo licha ya jitihada za kuhamasisha ulinzi jamii ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi wa polisi ngazi ya wilaya na mkoa.

Tunashauri kuwa kuna haja pia ya kupanga mkakati wa kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa Zanzibar kuhusu umuhimu na faida za kushiriki katika ulinzi shirikishi.

Bila kufanya hivyo, matukio ya uhalifu yanaweza kuongezeka na pia vituo vidogo vilivyofungwa kwa ajili ya kutumiwa na polisi jamii havitaweza kufanya kazi.

Vituo vidogo vya polisi vina umuhimu mkubwa kwa ulinzi na usalama wa raia na mali zao, kwa sababu viko karibu na wananchi, hivyo inakuwa rahisi kuwahudumia.

Tangu mpango wa ujenzi wa vituo vidogo vya polisi Tanzania Bara na Zanzibar ubuniwe na kutekelezwa chini ya Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Augustino Mrema, umekuwa ukielezwa kuwa na manufaa makubwa, kubwa likiwa ni kuhudumia wananchi wengi kwa ukaribu.

Tunaamini kuwa juhudi zitafanyika kuongeza idadi ya askari Zanzibar ili vituo vidogo vya polisi viendelee kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa katika miaka ya karibuni Zanzibar imekuwa ikikabiliwa na matukio mengi ya uhalifu, yakiwamo ya ujambazi wa kutumia silaha.

Suala lingine linalodhihirisha kuwa Zanzibar inahitaji askari polisi zaidi ni ongezeko la idadi ya watu ambayo imekuwa ikiongezeka kila uchao. Ongezeko la watu liinahitaji pia kuwapo uwiano na polisi.

Bila shaka mamlaka za juu za serikali zote mbili ya Zanzibar na ya Muungano zitakuwa na taarifa kuhusu changamoyo hiyo ya Jeshi la Polisi Zanzibar, hivyo zitaifanyia kazi.

Sisi tunaona kuwa suluhisho ya changamoto hiyo ni kuongeza idadi ya polisi kwa kuzingatia kuwa Zanzibar inahitaji polisi zaidi, na siyo kufunga vituo.

Habari Kubwa