Wazawa waangaliwe katika ujenzi wa uchumi

13Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Wazawa waangaliwe katika ujenzi wa uchumi

NI jambo lisilo na ubishi kwamba wazawa wana mchango mkubwa wa uchumi wa nchi kulinganisha na wawekezaji wa kigeni.

Katika kuliweka hilo wazi, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi, amesema uchumi wa nchi yoyote duniani hujengwa na wazawa, hivyo serikali inapaswa kuwaamini badala ya kuwakumbatia wawekezaji wa kigeni.

Akizungumza mjini Dodoma katika mkutano wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi nchini juzi, Dk. Mengi alisema iwapo viongozi watawaamini wawekezaji wazawa, ana imani kuwa dhamira ya serikali katika kukuza uchumi wa kati, kuelekea Tanzania ya viwanda, itafanikiwa.

Alisema nchi yoyote haiwezi kujengwa na wageni bali wazawa iwapo watapewa kipaumbele na serikali katika kujenga uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Dk. Mengi, malengo ya sekta binafsi na serikali ni yale yale yakiwamo kuondoa umaskini, kutoa ajira na kuwapa maisha bora wananchi wake, hivyo kuiomba serikali kuipa kipaumbele ili wazawa washiriki katika kujenga nchi yao, badala ya kuwaachia wageni.

Ni ukweli kwamba wazawa wanahitaji kupewa upendeleo katika ujenzi wa uchumi kwa kutilia maanani kuwa wawekezaji wazawa kupitia sekta binafsi wamekuwa wanatoa mchango mkubwa kutokana na kutoa ajira nyingi kwa wananchi na vilevile kulipa kodi ambayo inaipatia serikali mapato.

Hata hivyo, pamoja na mchango huo, sekta binafsi inakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwamo za kutokuaminiana kwa sekta hiyo na ile ya umma kama alivyobainisha Makamu Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte kwamba kutokana na kushindwa kulipwa madeni yao pale wanapofuatilia kudai na kusababisha wengi kufunga shughuli zao.

Nyingine ni upungufu wa ushirikishwaji unaohusu serikali na kutojali mikataba mbalimbali na kuchukuliwa kama uonevu pamoja na kutokuwa na uhakika wa umeme mkubwa viwandani.

Kadhalika, ongezeko la kero kutoka taasisi kadhaa za serikali zikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi (Osha) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Zimamoto ambazo zimekuwa zikidai fedha na kuonekana kama kodi.

Tunaamini kuwa kupitia mkutano huo wa majadiliano, serikali ambayo iliwakilishwa na viongozi wazito Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, itakuwa imesikia ombi la sekta binafsi la kutaka wazawa wapewe kipaumbele katika umiliki wa uchumi pamoja na changamoto zinazowakabili.

Ni matumaini yetu kuwa wataziwasilisha katika mamlaka husika na zitafanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na kuwaondolea vikwazo wafanyabiashara.

Baadhi ya changamoto zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu na wafanyabiashara kuwa zinawakwaza. Kwa mfano ya kutolipwa madeni yao kumewafanya wengi wao kufunga shughuli zao.

Kutokuwapo na uhakika wa umeme mkubwa viwandani ni changamoto nyingine ambayo serikali inapaswa kuitafutia ufumbuzi, ingawa ziko jitihada kubwa zinazofanyika za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kuzalisha umeme.

Hakuna ubishi kwamba sekta binafsi ndiyo injini ya uchumi wa kila nchi, hivyo serikali inapaswa kuiangalia kwa jicho la pili kwa kuijengea mazingira bora ili ishiriki katika ujenzi wa uchumi na kuwaletea wananchi maendeleo.

Tunaamini kuwa serikali haiwezi kuleta maendeleo peke yake bila kushirikiana na sekta binafsi, hivyo ni wakati mwafaka wa kujenga ushirikiano imara pamoja na kuaminiana na ikiwezekana uwapo utaratibu wa kuwa na majadiliano ya mara wa mara.

Habari Kubwa