Wauza mafuta wanaokaidi matumizi EFD wafungiwe

14Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Wauza mafuta wanaokaidi matumizi EFD wafungiwe

SERIKALI imeonekana kukosa uvumilivu kwa vituo vya kuuza mafuta nchini, kutokana na ukaidi wao wa kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD).

Kutokana na wauzaji hao wa mafuta kukaidi kwa muda mrefu kuzitumia mashine hizo kwa sababu wanazozijua wao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameiagiza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya ukaguzi nchi nzima ili kubaini wamiliki wa vituo vya mafuta wanaokiuka maagizo ya Serikali yaliyowataka wafunge EFD tangu mwaka jana.

Dk. Mpango alitoa agizo hilo juzi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mpango aliamuru kituo cha mafuta cha GBP kifungwe hadi hapo kitakapofunga mashine za EFD.

Waziri alitoa hatua hiyo baada ya kubaini kituo hicho hakikuwa kikitumia ipasavyo mashine za EFD. Kituo hicho chenye pampu nne za mafuta kilikutwa na mashine moja ya mkononi ya EFD.

Jambo hilo, alisema Dk. Mpango, husababisha wateja wengi kutopewa risiti, hivyo kuikosesha Serikali mapato yake na ni kinyume cha sheria za nchi.

Kampuni za mafuta licha ya kuhimizwa kwa muda mrefu tangu mwaka jana, zimekuwa zikikwepa matumizi ya EFD kwa sababu ambazo hawazielezi, lakini kinachoonekana ni kwamba lengo lao ni kukwepa kulipa kodi za serikali.

Wauzaji wa mafuta wamekuwa wakiweka mazingira ambayo yanawafanya wanunuzi kusahau kudai risiti za EFD na wengine kuona kuwa kudai risiti kutawagombanisha na wauzaji hao.

Mara nyingi wanunuzi wa mafuta hawadai risiti hizo kutokana na haraka ili kuepukana na foleni barabarani, hivyo wauzaji kuitumia fursa hiyo na kukwepa kulipa kodi ya serikali.

Kutokana na wauzaji mafuta kuendelea kukaidi kutoa risiti kwa lengo baya la kukwepa kodi ya serikali, kuna kila sababu kwa serikali kuchukua hatua mbalimbali za kupata mapato yake.

Miongoni mwa hatua hizo ni kuvifunga vituo vitakavyobainika na kuvifutia leseni, lakini pia itakuwa vizuri kama TRA itaweka utaratibu wa kuwakadiria wauzaji wa mafuta wote kiasi ambacho wanatakiwa kuilipa serikali hata kama watakaidi kutoa risiti za EFD ili malipo hayo wayalipwe kwa mkupuo mmoja sambamba na faini na wakishindwa basi wafungiwe leseni.

Ni jambo la aibu kuona Waziri wa Fedha akienda mitaani na kukimbizana na wauza mafuta vituoni kuhakikisha kama wanatumia EFD wakati mamlaka zinazowajibika na jukumu hilo zipo hususan TRA. Inapofikia hapo, ni lazima wananchi wahisi kuwa mamlaka kusika zimezidiwa nguvu na wauzaji wa mafuta.

Wamiliki wa vituo vya mafuta wanapaswa kujua kuwa wanawajibika kuheshimu, kutii na kufuata maelekezo ya serikali na sheria za nchi kwa ujumla na kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Kwamba, kama sheria ya kutumia EFD ilipitishwa na utekelezaji wake kuanza rasmi, hakuna kukaidi bali wanaweza kuwasilisha malalamiko au maoni kama kutakuwapo na changamoto ili zifanyiwe kazi.

Tunawashauri wamiliki wa vituo vya mafuta na wauzaji wao kuacha kukaidi kutoa risiti hizo kwa sababu mamlaka zikichukua hatua wao ndio watakaoathirika zaidi.

Tunaamini kuwa TRA itaendelea kutimiza majukumu yake ya kukusanya kodi kama sheria ya kuanzishwa kwake inavyoelekeza na kusimamia utekelezaji wa agizo lake la mwaka jana kwa vituo vyote vya mafuta nchini viwe vimefunga mashine za EFD ambazo zimeunganishwa moja kwa moja kwenye pampu kufikia Machi mosi, 2016.

Kutokana na hali hiyo, watakaoendelea kukaidi agizo hilo wafutiwe leseni zado za kuuza mafuta ili liwe fundisho kwa wengine wanaoendelea kukaidi.

Habari Kubwa