Watumishi waliojiendeleza toeni ushirikiano uhakiki

12Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Watumishi waliojiendeleza toeni ushirikiano uhakiki

SERIKALI imeendelea na utaratibu wa kuweka sawa kumbukumbu za watumishi wake katika mfumo, kwa lengo la kuwatambua.

Safari hii imewataka watumishi wenye kiwango cha elimu ya darasa la saba kuwasilisha haraka serikalini vyeti vyao vya kujiendeleza mpaka kidato cha nne.

Agizo hilo lilitolewa juzi na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alipokuwa akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, na kufafanua kuwa agizo hilo linawahusu watumishi walioajiriwa baada ya Mei 20, 2004.

Alisema watumishi walioajiriwa kabla ya tarehe hiyo wataendelea na nafasi zao na kama walijiendeleza wanahitajika kuwasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kurekebishiwa taarifa.

Hatua hiyo imechukuliwa kama sehemu ya utaratibu wa uimarishaji wa mfumo wa serikali ambao utasaidia kupata taarifa sahihi za watumishi na kupunguza ukubwa na gharama za uendeshaji wa serikali.

Kwa mujibu wa Kairuki, Waraka wa Serikali Namba Moja wa mwaka 2004, umetoa ufafanuzi wa utaratibu kwa watumishi walioajiriwa serikalini kwa kiwango cha darasa la saba kutakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya kidato cha nne ili kukamilisha taratibu za utumishi wa umma.

Agizo hilo la serikali halina nia mbaya kama alivyosema Waziri Kairuki, bali kuwaweka katika mfumo rasmi wa serikali watumishi wa umma walioajiriwa wakiwa na elimu ya darasa la saba, lakini baadaye wanajiendeleza hadi kidato cha nne.

Pamoja na kuwekwa katika mfumo wa kutambuliwa na serikali, pia taarifa zao muhimu zitawekwa katika mfumo huo, hivyo ni utaratibu mzuri na wenye tija kwao.

Kwa kuwa serikali ina utaratibu wa kumpandisha daraja pamoja na mishahara mtumishi aliyejiendeleza, inawezekana wale ambao hawakuwasilisha vyeti vyao baada ya kujiendeleza wananufaika kwa kupandishwa madaraja na madaraja.

Kama serikali imeona umuhimu wa kutoa agizo la kuwasilisha vyeti hivyo, bila shaka imebaini kuwapo kwa changamoto katika suala hilo.

Inawezekana kuwa kuna watumishi waliojiendeleza hadi kidato cha nne, lakini hawakuwasilisha vyeti kwa mwajiri ambaye ni serikali baada ya kuhitimu masomo kwa sababu zisizojulikana.

Kuna uwezekano pia watumishi hao hawakuwasilisha vyeti kutokana na kutojua kuwa wanatakiwa kufanya hivyo, hivyo agizo la Kairuki lina lengo la kuwakumbusha.

Wito wetu kwa watumishi hao ni kuwa ni vizuri wakatoa ushirikiano kwa serikali kwa kutimia agizo la kuwasilisha vyeti vyao ili utaratibu wa kuwaingiza katika mfumo uendelee na wao watambulike rasmi.

Wanapaswa kufahamu kuwa serikali inaendelea kuhakiki taarifa za watumishi wake na mchakato huo umegundua baadhi ya taasisi za kiserikali zina watumishi ambao taarifa zao hazijitoshelezi, nyingine siyo sahihi wakati zingine ni chafu.

Tunawahimiza wawasilishe vyeti katika muda mwafaka kwani bila kufanya hivyo, wanaweza kujikuta wakipoteza haki zao za msingi.

Pia kutotii agizo hilo la serikali kunaweza kuonekana ni ukaidi, hivyo baadaye kuchukuliwa kama watumishi wasio na sifa zinazotakiwa katika utumishi wa umma.

Ni wajibu wa makatibu na maofisa utumishi kuhakikisha wanarekebisha haraka kasoro hizo pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi za watumishi kuanzia siku waliyoajiriwa, elimu zao, michango ya hifadhi ya jamii na vyeo husika vya sasa kama alivyoagiza Waziri Kairuki.

Tunasisitiza kuwa watumishi wote waliojiendeleza kielimu baada ya kuajiriwa wakiwa na elimu ya darasa la saba watoe ushirikiano wa kutosha kwa serikali kwa ajili ya uhakiki wa vyeti vyao.

Habari Kubwa