Watakaopandisha nauli watumbuliwe

21Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Watakaopandisha nauli watumbuliwe

ZIKIWA zimebaki siku nne kabla ya kusherehekea sikukuu ya Krismasi na baadaye Mwaka Mpya, kuna malalamiko kuwa baadhi ya mabasi yanayofanya safari za mikoani yameanza kupandisha nauli.

Mbali na malalamiko hayo, baadhi ya mawakala wamenaswa wakiuza tiketi kwa bei ya juu kinyume cha nauli zilizopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

 

Tabia ya kupandisha nauli siku za kuelekea sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya imekuwapo muda mrefu kwa mabasi yanayofanya safari za mikoani.

Kupandisha nauli kila ifikapo wakati huu husababishwa na tamaa ya fedha ya wafanyakazi wa mabasi hayo kwa kushirikiana na mawakala.

 

Hupandisha nauli kutokana na kuongezeka kwa wasafiri ambao huenda katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya mapumziko ya sikukuu hizo.

 

Hata hivyo, jambo la kushangaza ni kuwa tabia hiyo imekuwa ikiendelea licha ya mamlaka mbalimbali kama Sumatra na Polisi kutoa onyo kwamba watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.

 

Inavyoonekana ni kuwa baadhi ya wafanyakazi wa mabasi hayo na mawakala wameshindikana kutokana na kukokutii maagizo na makatazo ya mamlaka za serikali kuhusiana na upandishaji wa nauli za mikoani kinyume cha viwango vilivyowekwa na Sumatra.

 

Mwarobaini wa vitendo hivyo kwa sasa uwe ni kwa mamlaka husika kuachana na tabia ya kuwabembeleza wakaidi hao wa sheria, kanuni na taratibu badala yake zichukue hatua stahiki mara moja bila kuangalia aliyefanya kosa hilo ni nani.

 

Kwa kuchukua hatua kali dhidi ya atakayekaidi nauli halali itakuwa dawa na fundisho kwa wengine ili waogope kuendelea na tabia hiyo wakidhani kuwa serikali inawaogopa.

 

Sisi tunaamini kabisa kwamba wanafanya hivyo makusudi mazima kwa kuwa wanayo nauli iliyopangwa na Sumatra. Wanaopanga nauli ya kwao wakati huu wanalo jambo wanalolijua wao.

 

Tunaamini hivyo kwa kuwa kipindi ambacho sio cha sikukuu mabasi yamekuwa yakitoza nauli elekezi ya Sumatra au chini ya hiyo kutokana na kutokuwapo mahitaji makubwa ya usafiri.

 

Ili kukabiliana na wakaidi hao wa sheria, tunaishauri Sumatra iache kuwabembeleza badala yake ianze kuchukua sheria mara moja na ikiwezekana kipindi hiki ambacho malalamiko kadhaa yameanza kutolewa na wasafiri na umma kwa ujumla.

 

Maofisa na watendaji wa Sumatra pamoja na Jeshi la Polisi kama wanataka kubaini ukweli kuhusu hilo wawe wanakwenda kufuatilia katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo kila siku na kuwauliza abiria kuhusu viwango vya nauli wanazotozwa kwa sasa.

 

Mbali na kupandishwa kwa nauli kiholela, pia tunazishauri mamlaka zetu kufuatilia kwa karibu usalama wa mabasi yanayotumika kwa sasa kusafirisha abiria kwenda mikoani.

 

Kutokana na mahitaji makubwa ya usafiri wakati huu, wenye mabasi kutokana na tamaa ya kuvuna fedha bila jasho, wamekuwa wakitumia hata mabasi yasiyo salama kusafirisha abiria.

 

Kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea ajali za kuhatarisha maisha ya watu. Dawa ya kuzuia matukio kama hayo ni Jeshi la Polisi kujipanga kwa kusambaza askari wake wa Kikosi cha Usalama Barabarani maeneo mengi ya barabarani kufuatilia magari yote yanayosafirisha abiria kwenda mikoani kama ni salama na yana vibali vya kusafirisha abiria.

 

Umuhimu huo unatokana na tabia iiyozoeleka kipindi hiki kila mwaka magari mengi ya kila aina yakiwamo madogo kusafirisha abiria kwenda mikoani.

Tunasisitiza kuchukuliwa hatua kuhakikisha usafiri wa mikoani unakuwa salama pamoja na hakuna watakaodiriki kutumia siku za sikukuu kupandisha nauli, vinginevyo watakaobainika watumbuliwe.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa