Wajanja wasifanye mradi katika upunguzaji bei za dawa, vifaa tiba

09Jul 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Wajanja wasifanye mradi katika upunguzaji bei za dawa, vifaa tiba

SERIKALI juzi ilitangaza neema kwa wananchi kutokana na kushusha bei za dawa muhimu kwa wastani wa asilimia 15 hadi 80, hatua ambayo itawapunguzia wananchi mzigo wa kubeba gharama za matibabu.

Uamuzi huo wa serikali ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kutaka kupunguzwa kwa bei za dawa na vifaa tiba ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata huduma za matibabu kwa urahisi.

Ahadi hiyo pia aliitoa wakati wa kampeni za kugombea urais mwaka 2015 kuwa serikali atakayounda inadhamiria kuboresha huduma za afya.

Katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, Rais aliagiza serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuagiza dawa moja kwa moja nje ya nchi na katika viwanda vya ndani badala ya kutumia mawakala ambao huongeza fedha zao, maarufu kama ‘cha juu’.

Kutokana na utekelezaji wa agizo hilo, Watanzania wengi watapata nafuu kubwa ya gharama za matibabu hususan katika ununuzi wa dawa ambazo zimekuwa zikiuzwa kwa gharama kubwa.

Ni wazi kwamba Watanzania wengi ni wa kipato cha chini na gharama za matibabu zimekuwa zikiwatesa hasa wanapopatwa na maradhi. Mtu anapokuwa na ugonjwa, mathalan, kwa kima cha chini anaweza kutumia si chini ya Sh. 50,000 iwapo hana bima ya afya, kiasi ambacho ni kikubwa kulinganisha na kipato chake.

Kutokana na punguzo hilo, Mtanzania huyo wa kawaida anaweza kupata matibabu kwa kutumia hata Sh. 15,000 au chini yake na hiyo itakuwa ukombozi mkubwa kwake. Zaidi ya hayo, upatikanaji wa dawa utakuwa wa uhakika kwa sababu dawa zitapelekwa moja kwa moja katika maeneo husika.

Kwa ujumla, kutokana na uamuzi na kuanza kutekelezwa kwa agizo hilo, serikali inastahili pongezi kubwa kwani kwa hatua hiyo, imeonyesha kwa dhati kwamba inawajali wananchi wake.

Licha ya kuwajali wananchi wake, serikali inatambua kwamba katika kipindi hiki ambacho inatekeleza azma yake ya kuelekea uchumi wa viwanda, suala la afya ni jambo la muhimu kwa kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana kama taifa halina rasilimali watu yenye afya.

Pamoja na ukweli huo, ni vyema wahusika wakatekeleza agizo hilo, hususan upatikanaji wa dawa kwa uhakika na kwa uwazi na baadhi ya watu wenye tabia ya udokozi, wasichukulie kama mwanya wa kujinufaisha. Tunasema hivyo kwa sababu wapo watu waliozoea kujinufaisha na miradi ya serikali kila inapoanzishwa. Kwa suala la dawa isiwe hivyo.

Aidha, kusijitokeze visingizio vya kiwango duni cha upatikanaji wa dawa au ukosefu wa baadhi ya dawa katika maduka ya dawa hususan kwenye hospitali kwani baadhi ya watumishi husingizia hivyo kwa lengo la kuwafanya wagonjwa kwenda kununua dawa husika kwenye maduka yao.

Ni imani kwamba suala hili litafanyika kwa ufanisi tangu uagizaji wa dawa, uhifadhi hadi usambazaji katika mikoa na wilaya ili wananchi wazidi kunufaika na mpango huu wa serikali ambao utaimarisdha afya za Watanzania na kukuza uchumi wa nchi.

Habari Kubwa