Vyama vionyeshe ustaarabu kampeni za Dimani, kata 22

06Jan 2017
Mhariri
Nipashe
Vyama vionyeshe ustaarabu kampeni za Dimani, kata 22

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Dimani Zanzibar zimeanza, baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) jana kuzizindua kwa upande wao huku Chama cha Wananchi (CUF) kilitarajia kuzindua Jumapili.

Uchaguzi huo utafanyika kutokana na kufariki dunia kwa aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ali Tahir, Novemba, mwaka jana mjini Dodoma.

Kampeni za CCM zilizinduliwa jana katika kiwanja cha Maungani, Dimani na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye alikuwa na viongozi kadhaa waandamizi wa CCM wa Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa upande wake, CUF ambacho ni chama kikuu cha upinzani Visiwani, kinatarajia kuzindua kampeni zake Jumapili, huku Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad, akitarajiwa kuzizindua.

Mbali na kampeni za Dimani, vyama kadhaa vyenye usajili wa kudumu vitashiriki uchaguzi wa marudio wa udiwani katika kata 22 nchini, utakaofanyika sambamba na uchaguzi mdogo wa Dimani. Marudio ya uchaguzi katika kata 22 Januari 22, yanatokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kufariki dunia kwa wagombea na kujiuzulu kwa waliokuwa wanashikiria udiwani.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, vyama kadhaa vitashiriki kwa kusimamisha wagombea katika uchaguzi mdogo wa Dimani na wa udiwani katika kata 22.

Tunaamini kuwa kupitia katika mikutano ya kampeni, wananchi watapata fursa nzuri ya kuwasikiliza wagombea na vyama vyao wakijinadi kuhusiana na mambo ya maendeleo watakayoyafanya ikiwa watachukuliwa.

Kwa kuwa mikutano ya kampeni ndiyo fursa pekee ya kuwawezesha wananchi kuwafahamu vizuri na kwa undani wagombea kwa maana ya uwezo wao, tunawashauri wananchi waipe kipaumbele mikutano ya kampeni kwa kujitokeza kuwasikiliza wagombea hao kuhusu mikakati yao, mipango na programu kuhusiana na watakavyopeleka maendeleo katika maeneo yao na jinsi watakavyosaidiana na wananchi kukabiliana na changamoto.

Ni kupitia kuhudhuria mikutano ya kampeni, wananchi watasikiliza sera, ilani, itikadi, mikakati na mipango ya vyama na mwishowe kuamua kuchagua chama ambacho watabaini kinaweza kuwaondolea changamoto na kuwapatia maendeleo.

Tunaamini vyama na wagombea wao wataitumia mikutano ya kampeni kuwaeleza wananchi kwa ufasaha mambo watakayowafanyia, badala ya kutumia majukwaa ya mikutano ya kampeni kudanganya, kupiga soga, blablaa sambamba na kutumia lugha za kejeli, matusi na kashfa dhidi ya viongozi wa vyama vingine na wa serikali.

Vile vile, tunatoa rai kwa wanasiasa, wafuasi wa vyama na wasio na vyama kuhakikisha wanajiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu. Kikubwa ni kuzingatia ratiba ya mikutano uliyoandaliwa na NEC pamoja na sheria za uchaguzi, kanuni na miongozo yake ikiwamo kufunga mikutano saa 12:00 jioni.

Kama kutakuwapo na malalamiko kutoka kwa wapigakura, vyama na wagombea yapelekwe vyombo husika ikiwamo NEC na Jeshi la Polisi, badala ya kujichukulia sheria mikononi.

Tunaamini Jeshi la Polisi litatekeleza jukumu lake la kuhakikisha kuna amani na utulivu katika maeneo yote ya uchaguzi na kutenda haki sawa kwa vyama vyote. Watu wote kuwa wastaarabu na kufuata sheria ndiyo njia pekee itakayofanikisha uchaguzi huo.

Habari Kubwa