Ushauri wa viongozi  wa dini uzingatiwe

26Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Ushauri wa viongozi  wa dini uzingatiwe

JUZI wakati wa ibada ya mkesha wa Krismasi na mahubiri ya jana ya maadhimisho ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo takribani miaka 2000 iliyopita, viongozi wa dini ya kikristo wakiwamo wachungaji, wainjilisti, mapadri na maaskofu walizungumzia mambo mbalimbali.

Mambo ambayo yanaiathiri jamii na kutoa ushauri kadhaa kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi. 

Wapo waliozungumzia suala zima la wajibu wa kila raia kutimiza wajibu wake wa kulipa kodi ya serikali ili iweze kupata uwezo wa kuwaletea maendeleo zikiwamo huduma muhimu za kijamii kama maji, afya, elimu na miundombinu.

Walisema kuwa bila raia kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, serikali haitaweza kuwaletea maendeleo hayo na watabaki katika mahangaiko ya umaskini. Viongozi hao pia waliwakumbusha wafanyabiashara wajibu wao wa kulipa kodi za serikali.

Askofu mmoja wa Zanzibar alisema aliwasisitiza watu wote umuhimu wa kulipa kodi akisema kodi ni haki ya lazima na kubainisha kuwa licha ya Serikali kuhimiza ulipaji wa kodi, lakini wapo wakwepaji wa kodi ambao baadhi yao ni wafanyabiashara wakubwa. Alisema wakwepaji kodi wanafahamika kuwa ni wafanyabiashara wakubwa na kwamba hawa ndio watumiaji na waharibifu wakubwa wa miundombinu ya nchi na kutoa mfano kuwa baadhi wanamiliki matrela yaliyokamatwa bandarini hivi karibuni. Alisema wale wanaodhani kuibia Serikali kupitia ukwepaji wa kodi sio dhambi wanakosea kwa kuwa hiyo ni dhambi kubwa kwa kuwa inaumiza kizazi cha sasa na cha baadae. Pendekezo lake ni kuwa serikali iwafilisi na kunyang’anywa leseni zao za biashara ili kuwaondolea wananchi wa kawaida mzigo wa umaskini.

 Wapo viongozi kadhaa waliozungumzia haja ya kuwawezesha vijana kwa njia mbalimbali za kupata ajira ikiwamo elimu ili waweze kuajiriwa au za kujiajiri ili kukabiliana na changamoto za maisha.

Suala la rushwa na ufisadi pia liligusiwa katika mahubiri na viongozi wengi huku wakiunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya vitendo hivyo. Baadhi waliishauri jamii kuunga mkono hatua hizo na kuwa na uvumilivu na subra wakati serikali ikiendelea kuchukua hatua dhidi ya mafisadi na rushwa.  Mchungaji alisema katika kudhibiti mafisadi, wananchi wa kawaida wataathirika akitolea mfano kuwa miti mikubwa inapong’olewa msituni lazima na miti midogo nayo itaumia. Katika kutimiza lengo la kudhibiti rushwa na ufisadi, wananchi wameshauriwa kuheshimu na kufuata utawala bora.

Kwa upande wake, serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano na Zanzibar ziweke mkazo katika ukusanyaji wa kodi kwa wakati ili  kupata maendeleo zaidi na kila mwananchi kupata huduma zinazostahiki.Aidha, suala la matumizi ya dawa za kulevya lilichukua nafasi kubwa na kushauri jamii ijiepushe na dawa hizo kwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha kuharibu maisha ya vijana.

Mmomonyoko wa maadili kwa watoto ulitajwa huku baadhi ya viongozi hao wakielekeza lawama kwa wazazi kwamba baadhi yao wanashindwa kutimiza wajibu wao wa kukaa kwa karibu na watoto wao na kuwapa malezi stahiki.

Mmoja wa maskofu alisema kuwa siku hizo malezi ya mtoto yanategemea mzazi na siyo jamii tofauti na iivyokuwa zamani ambapo mtoto alipofanya kosa alikuwa anaadhibiwa na mtu yeyote katika jamii.

Kadhalika, walihimiza kudumisha amani na upendo katika jamii. Tumefarijika na ushauri wa viongozi hao wa kiroho ambao una lengo la kujenga jamii bora na yenye furaha.

Tunachukua fursa hii kuishauri jamii mzima kuzingatia ushauri huo wa viongozi wetu wa dini kwa kuwa utasaidia kuijenga jamii yetu na kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri na salama pa kuishi. 

Habari Kubwa