Usafiri wa reli ya kisasa utaleta manufaa makubwa

14Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Usafiri wa reli ya kisasa utaleta manufaa makubwa

RAIS John Magufuli juzi alifanya tukio la kihistoria la kuzindua mradi mkubwa wa reli ya kisasa maarufu kama ‘standard gauge’ awamu ya kwanza unaoanzia jijini Dar es Salaam hadi Morogoro.

Tunaliita tukio hilo kuwa ni la kihistoria kwani ndoto za Watanzania kuwa na reli ya kisasa ambayo waliitamani kwa miaka mingi iliyopita imetimia.

Kutimia kwake kumefanikishwa kwa kiasi kikubwa na umakini wa serikai ya Rais Magufuli wa kutekeleza kwa vitendo ahadi walizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwa Watanzania wengi wenye kiu ya maendeleo bila shaka watakuwa wamefurahia kuzinduliwa kwa mradi huo ambao ujenzi wake kwa mujibu wa Rais Magufuli alivyosema katika hotuba yake ya uwekaji wa jiwe la msingi kwamba reli hiyo ilipaswa kuanza kujengwa mwaka 1961.

Ni kweli kwamba ujenzi wa reli hiyo umechelewa kwa kuwa ingekuwa imechochea maendeleo ya nchi kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, lakini pamoja na hali hiyo, Watanzania tuna haki ya kujivunia kuona umeanza.

Kingine ambacho Watanzania wanapaswa kujivunia ni jinsi serikali yao ilivyojipanga kwa kutoa kipaumbele katika ukusanyaji wa mapato yake na kuyaelekeza katika miradi ya maendeleo. Ukweli huo unathibitishwa na habari kwamba kiasi cha Sh. trilioni 2.8, zitakazotumika katika awamu ya kwanza ya ujenzi huo kutoka la Dar es Salaam hadi Morogoro ni za nchini.

Tunaipongeza serikali kwa umakini wake wa kutekeleza miradi mikubwa ambayo ina maslahi makubwa kwa taifa na inawagusa wananchi wengi, ikiwamo reli ya kisasa.

Kikubwa zaidi ni kutekeleza mradi huo kipindi kifupi baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani, licha ya kukuta changamoto kadhaa hususani ya serikali kutokuwa na fedha za kutosha.

Tunakubaliana na kauli ya Rais Magufuli kuwa sababu kubwa ilichangia ucheleweshaji wa ujenzi wa reli hiyo ni umaskini, lakini kwa upande mwingine, sababu hiyo isiendelee kutumika kwa kuwa itatumiwa na watu wasio na uzalendo na maendeleo ya taifa letu.

Tunasema hivyo kwa sababu Tanzania ni nchi iliyojaliwa rasilimali za kutosha yakiwamo madini, mifugo, maziwa, wanyamapori, ardhi yenye rutuba na sasa mafuta na gesi asilia.

Mapato yatokanayo na rasilimali hizo zikisimamiwa na kutumika vizuri yatasaidia kugharamia miradi mingine mikubwa ya maendeleo kama ujenzi zaidi wa barabara za kisasa, viwanja vya ndege, ujenzi wa hospitali, shule na miradi ya maji.

Mradi wa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa tunatarajia utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa taifa kwa kuwa utawawezesha abiria wanaotumia usafiri wa treni inayopita kwenye reli hiyo kutumia muda mfupi wa saa 7:40 kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na vile vile saa 2:50 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma.

Huo utakuwa ni ukombozi kwa kuwa usafiri wa reli kwa sasa licha ya kutokuwa wa kuaminika, lakini pia abiria wanatumia muda mrefu kufika wanakokwenda.

Faida nyingine ni treni kuwa na uwezo wa kubeba mizigo mikubwa pamoja na kurahisisha usafiri wa abiria kwa nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Kenya, Sudani Kusini na pia kukuza biashara za nchi hizo.

Watanzania pia watanufaika kwa ajira 600,000 zikiwamo ajira 300,000 za moja kwa moja, ambazo zitasaidia kupunguza changamoto ya umaskini.

Matarajio yetu ni kuwa mradi huo ambao utaleta manufaa makubwa kwa nchi yetu, utasimamiwa vizuri ili pamoja na mambo mengine, utumie fedha zilizopangwa na kukamilika kwa wakati.

Habari Kubwa