Umakini muhimu kwa askari wanyamapori

04Jan 2017
Mhariri
Nipashe
Umakini muhimu kwa askari wanyamapori

JANA vyombo vya habari kadhaa vilichapisha habari kuhusu tukio la askari watatu wa wanyamapori wa Pori la Akiba Swagaswaga wilayani Kondoa mkoani Dodoma, kukamatwa kwa tuhuma za kumuua kwa risasi mkazi wa kijiji cha Olimba Wilaya ya Chemba, kwa madai ya kubeba nyama pori.

Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa, alisema mkazi huyo aliuawa Jumamosi iliyopita katika kijiji cha Selya wilayani humo, na kwamba marehemu alikuwa akiendesha pikipiki huku akiwa amepakia kiroba kilichokuwa na sukariguru.

Kwamba askari wanyamapori hao walimhisi amebeba nyama pori na bila kumsimamisha na kumhoji, waliamua kutumia bunduki zao kumuua papo hapo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mambosasa, baada ya kufanya mauaji hayo, askari hao waliubeba mwili huo kwenye gari walilokuwa nalo pamoja na pikipiki ya marehemu na kiroba cha sukariguru, kisha kwenda kuutelekeza ndani ya pori hilo la Swagaswaga.

Aliongeza kuwa baada ya kuutelekeza mwili huo ndani ya pori hilo, walichukua pia pikipiki na kiroba na kuvificha kila kimoja mahali pake kwa lengo la kupoteza ushahidi wa tukio hilo.

Hata hivyo, alisema wakati askari hao wanafanya tukio hilo, walishuhudiwa na mwananchi mmoja wa kijiji hicho aliyekuwa amejificha porini na ndiye aliyetoa taarifa Kituo cha Polisi Kondoa kisha kuwakamata.

Tusingependa kulijadili tukio hilo kwa kuwa litafikishwa na kutolewa uamuzi na vyombo vya sheria, lakini tunawashauri askari wote wa wanyamapori katika mapori ya akiba na hifadhi za taifa kuongeza umakini katika utekelezaji wa majukumu yao ya kulinda wanyamapori ambao ni rasilimali muhimu kwa taifa letu.

Tunasema hivyo tukifahamu kuwa katika miaka ya karibuni matukio ya ujangili yameongezeka kwa kasi kubwa na kusababisha wanyamapori wengi kuuawa na majangili ambao wameunda mitandao mikubwa kwa lengo la kufanikisha malengo yao ya kujipatia fedha na kusababisha nchi kupoteza rasilimali ambazo zinachangia pato kubwa katika uchumi.

Hata hivyo, pamoja na ujangili kuwa ni janga la taifa, bado askari wa wanyamapori wanawajibika kutekeleza majukumu yao kwa umakini. Kikubwa zaidi kutambua kuwa kila binadamu ana haki ya kuishi ambayo imeainishwa katika katiba ya nchi.

Kwa hiyo kitendo chochote cha kumhisi mtu kwamba amebeba nyara za serikali na kumshambulia kwa silaha bila kumkamata, kumhoji na kumfikisha mbele ya vyombo husika vya sheria, ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Yapo mazingira ambayo askari hao wanaweza kutumia silaha za moto kukabiliana na majangili, hususani pale wanapoona wahalifu hao wana silaha kwa lengo la kujihami.

Vile vile, askari hao wamepata mafunzo ya kutosha ya utekelezaji wa majukumu yao, hivyo wanaelewa namna ya kuwatambua majangili na jinsi ya kukabiliana nao.

Kuna baadhi ya watu ambao wanakerwa na kasi kubwa ya ujangili nchini kiasi cha kupendekeza kuwa mtu akionekana eneo la hifadhi ya mapori ya akiba, apigwe risasi kwa kuwa ni jangili.

Tunaendelea kusisitiza kuwa hilo lisifanyike, bali taratibu zifuatwe kuanzia kujiridhisha bila kuacha shaka yoyote na kisha kumfikisha katika mkono wa sheria, vinginevyo watu wasio na hatia wanaweza kupotea uhai wao.

Tunawahimiza askari hao kutokuwa wazembe, badala yake wazingatie weledi wa kazi ili kuepuka kuwaumiza wananchi wasio na hatia.

Habari Kubwa