Tusiruhusu uingiaji holela wa wageni haramu nchini

29Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Tusiruhusu uingiaji holela wa wageni haramu nchini

BAADHI ya nchi jirani zimekuwa zikitajwa mara kwa mara kuwa raia wake wanaishi nchini kinyume cha sheria.

Nchi jirani ambazo Idara ya Uhamiaji inazitaja kuwa raia wake wanaongoza kwa kuingia nchini kinyume cha sheria, taratibu na kanuni ni za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Burundi.

 

Kwamba raia wa nchi hizo mbili wamekuwa wakiingia nchini kinyume cha sheria na kukutwa katika maeneo mbalimbali likiwamo jijini Dar es Salaam.

 

Mbali na jiji la Dar es Salaam linaloshika nafasi ya tatu kwa kukutwa na raia wengi wa kigeni waishio kinyume cha sheria, mikoa mingine inayotajwa na Idara ya Uhamiaji ni Kigoma inayoongoza na Kagera.

 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Msemaji wa Idara ya Uhamiaji, Mrakibu Ally Mtanda, kuna wahamiaji haramu 7,033 waliokamatwa nchini katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, mkoa wa Kigoma uliongoza kwa kuwa na wahamiaji hao 388.

 

Mikoa mingine inayotajwa kwa kuwa na matukio mengi ya kukutwa na wahamiaji haramu na idadi ikiwa kwenye mabano ni Kagera iliyokutwa na wahamiaji haramu 347, Dar es Salaam (198), Tabora (163), Mara (85), Shinyanga (84), Njombe (31) na Morogoro (28). Wengine walikamatwa katika maeneo mengine.

 

Sababu anayoutajwa Mtanda kwamba inasababisha Mkoa wa Kigoma kuongoza kwa kuingiza wahamiaji haramu wengi kuliko mikoa yote, ni   kupakana na nchi zenye vurugu migogoro ya kisiasa ya mara kwa mara na vita.

 

Katika kipindi hicho, wageni waliokamatwa wakiingia nchini kinyume cha sheria na utaratibu kutoka katika nchi za Ethiopia na Somalia walikuwa 858 na wengi wao huwa na kawaida ya kuingia nchini kwa kupitia njia za panya kwenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Tanga, wakiwa safarini kwenda kutafuta maisha Afrika Kusini na kwingineko kupitia nchi hiyo.

 

Baadhi ya maeneo ambayo wahamiaji hao haramu hukamatwa kutokana na operesheni mbalimbali za kuwasaka huwa ni kwenye vituo vya mabasi, barabarani, kwenye vyombo vya usafiri, nyumba za kulala wageni, viwandani na pia mashambani.

 

Taarifa za Uhamiaji zinatoa picha kwamba kuna kasi kubwa ya kuingia kwa wahamiaji wengi haramu nchini, hivyo kuwapo umuhimu wa kuchukua hatua za dhati na endelevu kudhibiti hali hiyo.

 

Umuhimu huo unatokana na athari zitokanazo na uwapo wa wahamiaji haranu kwa nchi, kubwa zaidi ikiwa kuhatarisha usalama.

 

Tunapaswa kujiuliza ni sababu zipi zinawasukuma wageni kuingia nchini bila kufuata sheria kama kweli wana mahitaji ya kuingia nchini.

 

Kama mtu anaamua kuingia kupitia njia za panya basi anakuwa na sababu zingine ambazo ni mbaya na ni tishio kwa amani na usalama wa nchi aliyoingia.

 

Tunapongeza hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa na mamlaka husika dhidi ya wahamiaji haramu wanapobainika kuingia nchini, ikiwamo

 

kufikishwa mahakamani na kuadhibiwa kwa kufungwa, kulipishwa faini na wengine kurudishwa kwenye nchi zao.

 

Hata hivyo, kwa upande wetu tunaona kuwa njia pekee ya kupunguza kasi ya wahamiaji haramu nchini ni kuweka udhibiti katika maeneo yote ya kuingilia nchini ya mipakani, viwanja vya ndege, bandari na njia nyingine za ‘panya’.

 

Tunaamini kuwa njia hii inaweza kudhibiti tatizo hili kwa kiwango kikubwa kwa kuzingatia kuwa wakishaingia nchini inakuwa rahisi kufichwa na wahalifu wenzao, ndugu, jamaa na marafiki.

 

Kadhalika, kuna umuhimu wa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka za serikali wanapowahisi baadhi ya watu kuwa ni wageni haramu sambamba na vyombo vya serikali kuwa na mipango endelevu ya kudhibiti wahamiaji haramu.

 

 

 

Habari Kubwa