TFF itambue ushindi michezo mingi ya kimataifa unaipandisha TZ FIFA

08Jul 2017
Mhariri
Nipashe
TFF itambue ushindi michezo mingi ya kimataifa unaipandisha TZ FIFA

TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' jana ilikamilisha ushiriki wake kwenye michuano ya kombe Cosafa inayomaliza kesho nchini Afrika Kusini.

Taifa Stars ilishiriki michuano hii kama mgeni mwalikwa kwa kuwa si mwanachama wa baraza la vyama vya soka kusini mwa Afrika (Cosafa).

Hii ni mara ya pili kwa miaka ya karibuni kualikwa kushiriki katika michuano hii ya Cosafa.

Lakini mashindano ya mwaka huu Taifa Stars imeacha jina au tunaweza kusema 'imeweka heshima' na kuwaacha hoi wenyeji wao ambao ndio wenye mashindano haya.

Stars imeonyesha uwezo mkubwa na kuwa miongoni mwa timu zilizokuwa zikiogopwa kila siku zilivyokuwa zinazidi kwenye kwenye michuano hii.

Kitendo cha kuifunga Afrika Kusini kwenye hatua ya robo fainalina kuivua ubingwa hakikutarajiwa na watu wengi si tu kwa timu shiriki bali pia kwa watanzania tuliobaki nyumbani tukifuatilia kwenye televisheni michuano hii.

Pamoja na mafanikio hayo ya Taifa Stars kwenye michuano hii ya Cosafa, Nipashe tunapenda kulikumbusha Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwa kupanda kwa viwango kwa nchi yetu kunategemea zaidi kufanya vizuri kwenye michuano ya Kimataifa pamoja na mechi za kirafiki za kimataifa zinachezwa kwenye kalenda ya FIFA.

Kwa mfano, katika viwango ambavyo vimetolewa wiki hii na FIFA kwa ajili ya mwezi Juni, Tanzania imepanda kwa nafasi 25 kutoka nafasi ya 139 mwezi Mei mpaka kufikia 114 mwezi Juni.

Nipashe inafahamu mafanikio haya ya kupanda kwa nafasi 25 kumetokana na Taifa Stars kufanya vizuri kwenye mechi zake za kimataifa zilizochezwa katika kipidi hicho.

Ni vyema sasa TFF ikashikilia mafanikio haya kwa kuhakikisha Taifa Stars inacheza mechi nyingi za kirafiki pamoja na ile ya michuano ya kimataifa na kupamaba kupata ushindi ili Tanzania iendelee kupaa kwenye viwango vya soka vya FIFA.

Baada ya ushiriki wa Taifa Stara kwenye Cosafa, kwa sasa inakabiliwa na mchezo wa kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wanaocheza soka la ndani (CHAN) dhidi ya Rwanda.

Mchezo huu utachezwa Januari 15 mkoani Mwanza, Nipashe tunaamini ushindi katika mchezo huu unaweza ukatoa nafasi kwa Tanzania kupanda zaidi endapo itaibuka na ushindi.

Hivyo, Nipashe tunaikumbusha TFF kuelekeza nguvu kwenye mchezo huu kwa kuwa ushindi licha ya kuwa utatupandisha kwenye viwango lakini pia utatupa nafasi nzuri ya kusonga mbele katika mchakato wa kuwania kufuzu kwenye michuano hiyo ya CHAN.

Nipashe tunaipongeza TFF kwa sababu kufanya vizuri kwa Taifa Stars kwenye Cosafa pia kumechangiwa na namna wanavyojitahidi kuiandaa timu.

Kikubwa wasichoke na badala yake waongeze juhudi na maarifa katika kuandaa timu zetu za Taifa zinapokuwa zikijiandaa kushiriki katika michuano ya kimataifa.

Na hiyo isiwe kwa Taifa Stars peke yake, bali hata kwa timu nyingine za Taifa kama ilivyokuwa kwa Serengeti Boys ambayo ilishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika ya U-17.

Habari Kubwa