Tatizo linaloikumba MOI liwe chachu ya kubadili fikra

08Jan 2017
Mhariri
Nipashe Jumapili
Tatizo linaloikumba MOI liwe chachu ya kubadili fikra

KATIKA toleo la jana la gazeti hili, kulikuwa na habari kwamba Taasisi ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI) imeanza kuelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa kutokana na ongezeko la majeruhi wa ajali kila siku, wakiwamo wale wasio na ndugu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa katika wodi za taasisi hiyo, kuna zaidi ya wagonjwa 4,000 waliofikishwa kutokana na ajali mbalimbali zikiwamo za pikipiki, maarufu kama bodaboda, bajaji na magari.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa taarifa hiyo, inasababisha kukwama kwa juhudi za taasisi na serikali kwa ujumla kuboresha huduma kwa wagonjwa.

Sababu kubwa ya kuwapo kwa mrundikano huo wa wagonjwa kupita kiasi ni baadhi ya wanaofikishwa hospitalini hapo kukaa muda mrefu baada ya kupata matibabu na kuwa nafuu, kuendelea kubaki wodini kwa kile kinachoelezwa kuwa hawana ndugu.

Licha ya mrundikano huo, imeelezwa kwamba gharama za matibabu nazo zinaongezeka na kuwa mzigo mkubwa kwa taasisi kwani wale wanaodai kutokuwa na ndugu, wamekuwa wakitibiwa bure.

Hatua hiyo inaongeza mzigo kwa taasisi hivyo kutumia fedha nje ya kasma yake.

Pamoja na kuwapo kwa taarifa za baadhi yao kukosa ndugu, imebainika kuwa miongoni mwao wanao ndugu tena jijini Dar es Salaam na wanajaribu kujificha kutokana na kukwepa kuchangia gharama.

Habari zilizotolewa na ofisi ya uhusiano ya taasisi hiyo zilibainisha kwamba baadhi ya ndugu wa wagonjwa hao, hufika kuwaona kwa kujificha kwa kuogopa kuwa iwapo watabainika wanaweza kutwishwa mzigo wa kuwahudumia. Baadhi ya ndugu hao wamedaiwa kwenda kuwaangalia wagonjwa hao kwa kuvizia ili wasijulikane na uongozi wa MOI.

Kama vile haitoshi, kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo, hata pale wagonjwa hao wanapopata nafuu au kupona na kurejeshwa nyumbani kwa gharama za MOI, baadhi ya ndugu wamekuwa wakikataa kuwapokea kwa madai kuwa wametengwa na jamii kwa sababu mbalimbali.

Kulingana na utamaduni wa Kitanzania, kitendo kinachofanywa na ndugu wa wagonjwa hao si cha kiungwana kwani kinatupeleka katika utamaduni ambao haujawahi kuwapo tangu kuanzishwa kwa misingi ya taifa hili.

Kitendo cha kukwepa kujitambulisha kwa sababu ya kukwepa gharama za kumhudumia ndugu kwa ajili ya matibabu hakikubaliki hata kidogo.

Ni vizuri Watanzania wakabadilika na kurejea katika misingi ya kupendana na kuheshimiana ikiwamo kuwajali ndugu na jamaa, hususan wanapokumbwa na matatizo mbalimbali.

Aidha, ni jambo la ajabu kuona kwamba Watanzania wakishindwa kushiriki katika masuala ya kijamii kama vile kusaidia wagonjwa, lakini wako mstari wa mbele kuchangia mamilioni ya fedha katika sherehe zikiwamo harusi. Hata wakati wa misiba watu wamekuwa mstari wa mbele kutoa michango, lakini wanalipa kisogo suala la ugonjwa.

Umefika wakati sasa kubadilika na kusaidia ndugu wanaokumbwa na matatizo kama wanaolazwa na kutibiwa MOI kwa sababu hakuna mwanadamu ajuaye kesho yake kama atakuwa mzima au la.

Wanaopata ajali na kupelekwa katika taasisi hii ni ndugu au jamaa zetu ambao tunaishi nao au tuna nasaba nao, hivyo kutowasaidia ni kuwanyanyapaa.

Ni vyema Watanzania wakabadili mtazamo wao kimaisha kwa kuacha kuchangamka na kutoa michango mingi kwenye sherehe na kugeukia shughuli za maendeleo kama afya na elimu pamoja na kusaidia wahitaji, wakiwamo wagonjwa.

Katika nchi jirani ya Kenya, kumekuwa na matangazo mbalimbali ya watu kuitisha hafla za uchangiaji, maarufu kama harambee, pindi mtoto anapofaulu kujiunga na masomo ya sekondari au chuo na mmojawapo anapotakiwa kupatiwa matibabu ndani au nje ya nchi.

Kutokana na mfano huo, ni wakati mwafaka kwa Watanzania kubadilika na kufuata nyayo za majirani ambao bila kujali kama ni msiba au maendeleo, wamekuwa mstari wa mbele kuchangia fedha na kusaidiana. Huo ndio undugu hasa unaotakiwa na si kujaliana katika sherehe na misiba mtu akiwa amefariki dunia.

Habari Kubwa