Tahadhari muhimu maji Mto Msimbazi

13Jul 2017
Mhariri
Nipashe
Tahadhari muhimu maji Mto Msimbazi

IMEBAINIKA maji ya Mto Msimbazi yanayotumiwa kwa shughuli mbalimbali na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam siyo salama kwa viumbe hai

Taarifa hizo zimebainishwa na uchunguzi wa awali uliofanywa kuhusiana na maji yanayotiririka katika Mto Msimbazi. Uchunguzi huo unabainisha maji hayo yamechafuliwa na huua viumbe hai kutokana na kukosa hewa ya oksijeni.

Hayo yalibainishwa juzi na Meneja Maabara wa Mazingira, Wakala wa Maabara wa Mkemia Mkuu wa Serikali, Emmanuel Gwae, wakati wa ziara ya Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina.

Gwae alisema ili kujua kiwango cha uchafuzi wa maji hayo, ni lazima wapime kipimo cha oksijeni ambapo wamekuta zipo pointi 3.3, kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na kinachotakiwa cha 6 kwenda juu na kuwa maji hayo hayawezi kuwezesha viumbe kuishi kwenye maji kwa kuwa yamechafuka kwa kiwango cha hewa.

Taarifa hizo za uchunguzi wa awali zinazobainisha kuchafuliwa kwa maji hayo, zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa na wakazi wote wa Jiji la Dar es Salaam, kutokana na kutumia maji ya mto huo.

Tunasema kuwa asilimia kubwa ya wakazi wa jiji hilo ni watumiaji wa maji hayo kwa kuwa mboga za aina mbalimbali wanazokula zinalimwa kwa kutumia maji ya Mto Msimbazi.

Kama maji hayo yameathirika kama uchunguzi wa awali ulivyobainisha, ni wazi kuwa uwezekano wa watumiaji wa maji hayo kwa njia mbalimbali kama kuoshea vyombo, mboga na mengine kuwa wameathirika.

Tunampongeza Mpina kwa hatua yake ya kuagiza maji hayo kupimwa ili kujiridhisha kama ni salama ama la kwa watumiaji. Zimekuwapo taarifa za uvumi kwa miaka mingi kuwa maji ya mto huo sio salama kutokana na kuchafuriwa.

Katika kufuatilia taarifa hizo za uvumi, gazeti hili takribani miaka mitatu iliyopita, lilichapisha ripoti maalum iliyofichua jinsi walaji wa mboga za majani jijini Dar es Salaam walivyo hatarini kutokana na mboga hizo kuzalishwa kwa kumwagiwa maji yenye kemikali.

Katika ripoti hiyo ilieleza jinsi wakazi hao walivyo katika hatari ya kupatwa na magonjwa makubwa kama saratani, utasa, kupoteza uwezo wa kuona, kuharibu ubongo, maini na figo kutokana na matumizi ya mboga za majani zinazolimwa kwa wingi katika mabonde ya jiji hilo hususani Msimbazi.

Pia hatua ya Mpina ya kuelekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kupima ubora wa maji katika mito ya Dar es Salaam kutokana na uchafuzi wa mazingira unaoendelea ni nzuri na yenye tija kwa kuwa mito mingi imekuwa ikichafuriwa hususani na wenye viwanda.

Agizo lake la kupima maji ya mito ya Msimbazi, Mlalakua, Kibangu, Ng’ombe na Kijitonyama ambayo imekuwa ikitumiwa na wenye viwanda kuelekeza maji yao kutokana na kutokuwa na mfumo wa maji taka, litawezesha kupatikana ukweli kama maji hayo yako salama kwa matumizi ya viumbe hai, wakiwamo binadamu.

Tunashauri kuchukuliwa tahadhari baada ya taarifa ya awali ya uchunguzi kubainisha kuwa maji ya Mto Msimbazi yamechafuliwa. Jambo la msingi ni wananchi kusitisha shughuli za uchumi katika mto huo, zikiwamo kilimo cha umwagiliaji kinachofanyika pembezoni na uvuaji samaki.

Vile vile watumiaji wa mboga za majani zinazolimwa Mto Msimbazi wanapaswa kusitisha kuzinunua kwa lengo la kunusuru afya zao.

Ni matumaini yetu kuwa pamoja na tahadhari, Aidha, serikali itatoa uamuzi baada ya matokeo ya uchunguzi huo utakaofanywa na ofisi ya Mkemia Mkuu, Bonde la Mto Wami, Shirika la Viwango (TBS) na Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa siku 14 na kuwasilisha ripoti.

Habari Kubwa