Taarifa vichanga 10,000 kukutwa na VVU zinatisha

22Dec 2017
Mhariri
Nipashe
Taarifa vichanga 10,000 kukutwa na VVU zinatisha

KUNA taarifa za kutisha ambazo hata hivyo, zimethibitishwa na serikali kwamba watoto 10,000 huzaliwa kila mwaka wakiwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Aliyebainisha kuhusu janga hilo linaloshtua na kutisha kwa nchi yetu ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

 

Alibainisha hayo juzi katika hafla ya makabidhiano ya majengo ya Chuo cha Uuguzi Mirembe mkoani Dodoma na kutoa wito kwa jamii kuwa zinahitajika jitihada kubwa zaidi katika kukabiliana na tishio hilo.

Ummy alisema idadi hiyo ni tishio na yeye kama waziri mwenye dhamana ya afya inamkera, hivyo kuahidi kwamba serikali itahakikisha jitihada za makusudi zinafanyika kukabiliana na kupunguza tishio hilo.

 

Pamoja na kwamba idadi hiyo kubwa ya watoto wanaozaliwa kukutwa na maambukizi ya VVU kutisha, swali la msingi la jamii kujiuliza ni kitu gani kinachangia hali hiyo?

Majibu ya haraka yanayoweza kutolewa ni kuwa bado kuna kasi kubwa ya maambukizi ya VVU katika nchi yetu, ingawa takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa maambukizi hayo yanapungua.

Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Desemba Mosi mwaka huu, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aliyekuwa mgeni rasmi, alisema maambukizi ya VVU nchini yamepungua.

Makamu wa Rais alisema utafiti umeonyesha kupungua kwa kasi ya maambukizi ya Ukimwi kutoka asilimia 5.1 ya mwaka 2011/2012 hadi kufikia asilimia 4.7. Alisema kuwa hiyo inatokana na juhudi za pamoja kati ya serikali, wananchi na wadau mbalimbali ambao wamejikita katika kutoa elimu na huduma za masuala ya Ukimwi.

Hata hivyo, Samia alisema kuwa kupungua kwa kiwango cha maambukizi hakumaanishi kuwa Ukimwi umeisha, bali ni matokeo ya jitihada hizo za serikali na wadau wengine wakiwamo wananchi katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.

 

Jambo la msingi ni kuwa inapaswa kueleweka kwa kila mtu kuwa Ukimwi bado upo na kasi ya maambukizi ya VVU itaendelea kuwapo na kuzidi kupoteza nguvukazi ikiwa hatua zinazostahiki na endelevu hazitachukuliwa.

 

Tunaweza kudhibiti tishio la watoto wengi kuzaliwa na VVU ikiwa kina mama watakuwa na utamaduni wa kupima kabla ya kupata ujauzito ili kumuepusha maambukizi mtoto.

 

Vituo na watoa huduma za afya hawanabudi kutoa ushauri wa mara kwa mara kwa wajawazito ambao watabainika kuwa wameambukizwa ili kuchukua tahadhari ikiwamo kupewa dawa za kupunguza makali na tahadhari nyingine za kuchukua.

 

Elimu na ushauri yanapaswa kuwa mambo muhimu na ya kuzingatiwa na wajawazito ambao watagundulika kuambukizwa VVU.

 

Kwa kuwa serikali imelibaini tishio hilo na kuahidi kuchukua hatua kama alivyosema Waziri Ummy, ni matarajio yetu kuwa itatekeleza haraka na kwa umakini mkubwa ili kunusuru maisha ya watoto hao ambao ni tegemeo la Taifa la baadaye kama nguvukazi yake.

Pamoja na ahadi ya serikali ya kuendelea na mipango na mikakati ya kuhakikisha tatizo la watoto kuzaliwa wakiwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi linakwisha, kila mmoja bila kujali kama ni mwanaume au mwanamke katika jamii pia anapaswa kujua kuwa ni jukumu lake kuchukua tahadhari kujiepusha na maambukizi ya VVU.

 

Ulazima huo unatokana na ukweli kwamba ugonjwa wa Ukimwi bado ni janga kubwa kwa Taifa na Dunia kwa ujumla kwa kuwa hadi sasa haujapata tiba wala dawa.

Kupima ni suala muhimu kwa kuwa kunamwezesha kila mmoja kujua afya yake. Kama kuna mwanamama atajikuta ameambukizwa ajiepushe kubeba ujauzito ili asijifungue mtoto mwenye VVU.

 

 

Habari Kubwa