Soka 2017 tumepoteana, tunataka mafanikio 2018

01Jan 2018
Mhariri
Nipashe
Soka 2017 tumepoteana, tunataka mafanikio 2018

KWANZA kabisa, Nipashe tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuumaliza mwaka 2017 salama na kuuanza mwaka 2018, tukiwa bukheri wa afya.

Tunatambua wazi ni wengi tulianza nao mwaka jana, lakini kwa mapenzi yake Mola, wametangulia mbele ya haki, hivyo sisi ni nani hasa hata tusimshukuru Mungu kwa kuona mwaka huu mpya.

Hata hivyo, wakati leo tukiuanza mwaka mpya wa 2018, tunapenda kuwakumbusha wadau wa soka nchini na michezo yote kwa ujumla kufanya tathmini ya malengo yetu yaliyopita na kuanza kuandaa mikakati madhubuti ya kufanikiwa pale ambapo tulishindwa kupafikia, lengo likiwa ni kukuza michezo hapa nchini.

Kwa upande wa mchezo wa soka unaoongoza kwa kupendwa zaidi duniani, tukiwa kama wadau wakubwa tunakiri hatukupata mafanikio tuliyotarajia kwa mwaka 2017.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba kwa ngazi ya timu ya Taifa, tumeshuhudia timu zetu zote zikishindwa kufuzu michuano mikubwa kama Kombe la Dunia, michuano ya CHAN, huku pia timu ya Kilimanjaro Stars ikitia aibu kutokana na kuambulia sare moja tu na kupigwa mechi zingine zote kwenye michuano ya Kombe la Chalenji iliyomalizika jijini Nairobi, Kenya mwezi uliopita.

Pengine mafanikio makubwa kwetu kwa mwaka jana, labda  tunaweza kujivunia timu ya Taifa ya U-18 'Serengeti Boys' kufanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki fainali za vijana za Afrika zilizofanyika nchini Gabon.

Hata hivyo, Serengeti Boys', haikufanya vizuri kutokana na kushindwa kufuzu fainali za Dunia kwa umri huo kupitia michuano hiyo, ambazo baadaye zilimalizika kwa England kutwaa ubingwa wa Dunia.

Lakini pia, kamwe, hatuwezi kuyabeza mafanikio haya, kwani hii ni mara ya kwanza Tanzania kushiriki michuano hii ya vijana kwa Afrika, ikiwa ni baada ya miaka mingi kuhaha kupata nafasi hiyo.

Lakini pia tumeshuhudia klabu zetu za soka zilizoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga na Azam FC, zikishindwa kuiwakilisha nchi vema kimataifa.

Hivyo, ni vyema sasa klabu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na wadau wengine kujipanga vyema kwa mwaka huu wa 2018 kuhakikisha wanaweka malengo na kuyatimiza.

Kwa sasa Tanzania tunasaka tiketi ya kushiriki fainali za Afrika (AFCON) za mwaka 2019, ni vyema sasa kuweka mkazo katika maandalizi na michezo yetu ya kusaka tiketi na kuacha porojo.

Tunalazimika kulizungumza hilo kutokana na ukweli kwamba Taifa Stars imeanza kwa kujisuasua katika mechi hizo za kuwania kufuzu AFCON kutokana na kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Lesotho.

Hivyo kuna hatari ya kushindwa kufuzu michuano hiyo ambayo kwa mara ya kwanza Tanzania ilishiriki mwaka 1980.

Tunaamini waliofanikiwa, hawakupita njia za mkato, walijipanga na kuweka mikakati ambayo walihakikisha wanaitimiza na sasa hivi wapo mbali kisoka kuliko sisi.

Miaka ya nyuma nchi kama Cap Verde, Ethiopia, Sudan na hata Libya hazikuwa na maendeleo makubwa katika soka, nyingi tulikuwa nazo sawa au nyingine tuliziacha mbali.

Tunawatakia wanamichezo na Watanzania wote kwa ujumla kheri ya Mwaka Mpya 2018 katika kujipanga kutekeleza majukumu yao.

Habari Kubwa