Sakata Simba, Kagera Sugar aibu kwa TFF

17Apr 2017
Mhariri
Nipashe
Sakata Simba, Kagera Sugar aibu kwa TFF

KESHO Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), inatarajia kukutana kwa lengo la kupitia upya uamuzi uliotolewa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72.

Hatua hiyo imekuja ikiwa leo ni siku ya tano baada ya Kamati ya Saa 72 kuipa Simba pointi tatu kufuatia kukata rufani dhidi ya Kagera Sugar kumchezesha mchezaji Fakhi Mohammed ambaye anadaiwa kuwa na kadi tatu za njano.

Taarifa iliyotolewa juzi ilieleza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ina mamlaka ya kutafsiri sheria na kanuni za mpira wa miguu nchini kama ilivyoainishwa kwenye katiba na sehemu ya utangulizi ya kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Umuzi wa kamati hiyo kukutana kunatokana na ombi la timu ya Kagera Sugar ambayo imeomba kupitiwa upya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Saa 72, ilitoa matokeo mapya ya mchezo kati ya timu hiyo na Simba uliofanyika Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Katika mchezo huo, Kagera Sugar ilishinda mabao 2-1, lakini Simba ilikata rufaa ikidai kuwa Kagera Sugar ilivunja kanuni ya 37 (4) ya Ligi Kuu kwa kumchezesha mchezaji Fakhi Mohammed ambaye alidaiwa kuwa na kadi tatu za njano, hivyo ikaadhibiwa kwa mujibu wa kanuni ya 37 (37).

Katika taarifa ya wito iliyotolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kwenda kwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Ahmad Yahaya, kikao hicho pia kitawahusisha waamuzi, maofisa wa bodi hiyo na kamishna wa mchezo huo.

Na kwamba kila mmoja atatakiwa kufika na nyaraka muhimu kuhusiana na mchezo kati ya Kagera Sugar dhidi ya African Lyon, ambao Kagera Sugar inapinga kuwa Mohammed hakuonyeshwa kadi ya njano.

Nipashe tunaona hatua hiyo ni sawa na TFF kulitia doa soka la Tanzania kutokana na ukweli kwamba suala la rekodi za kadi si la kuhitaji waamuzi husika kwenda na ushahidi wa nyaraka muhimu kwani zilipaswa kuwa katika kumbukumbu la shirikisho hilo.

Tunasema hivyo kwa sababu mara baada ya mechi kumalizika waamuzi hukabidhi ripoti ya mchezo ambayo hujumuisha kila kitu kilichotokea ikiwamo wachezaji walioadhibiwa kwa kadi, iweje leo hadi kuitisha tena kamati huku wakisema ina wajibu wa kutafsiri sheria na kanuni ambazo ndizo zilizotumika kuipoka Kagera pointi.

Mathalani waamuzi husika wakiwa hawajazitunza kumbumbuku hizo, je TFF itatumia ushahidi gani kutenda haki.

Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka Simba ambao wanadai kuwa hatua inazochukua TFF zinatokana na presha kubwa kutoka kwa watani zao, Yanga, hata hivyo, sisi hatutaki kuamini katika hilo ila kuona haki ikitendeka.

Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa timu kupokwa pointi kwani Simba pia iliwahi kukumbwa na mkasa kama huo tena ilipocheza dhidi ya Kagera Sugar Januari 3, 2006 na kushinda1-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu.

Hata hivyo, Oktoba ikabainika kuwa Simba ilimchezesha Mussa Hassan Mgosi akiwa na kadi tatu za njano, hivyo ikapokonywa pointi tatu na mabao mawili, na kutoa nafasi kwa Yanga kutwaa ubingwa msimu huo.

Kadhalika, Yanga katika mismu 2013/14 ilipokwa pointi na kupewa Coastal Union baada ya kushinda 1-0 Machi 31, 2012, lakini iKifanya kosa kwa kumchezesha beki Nadir Haroub 'Cannavaro' akiwa na kadi nyekundu.

Timu nyingine iliyowahi kufaidika na pointi za mezani ni Mbeya City katika msimu wa 2015/16 baada ya Azam FC kuwachapa 3-0, lakini ikitenda kosa kwa kumchezesha Erasto Nyoni akiwa na kadi tatu za njano. Mifano hiyo itasaidia haki kutendeka na wadau kutambua si mara ya kwanza timu kupokwa pointi.

Habari Kubwa